Waendesha mashtaka wa baraza la wawakilishi wamefunga hoja zao katika kesi ya mashtaka dhidi ya Donald Trump, kwa kuliomba baraza la seneti kumtia hatiani kwa kuchochea shambulio baya la Januari 6 dhidi ya bunge.

Wasimamizi wa mashtaka hayo kutoka Baraza la Wawakilishi wamefunga kesi yao baada ya siku mbili za hoja zilizohusisha maneno ya Trump mwenyewe, na masaa kadhaa ya kuonyesha picha za video kutoka shambulio dhidi ya makao ya bunge na wafuasi wa Trump, ambao walikuwa wanataka kuzuwia zoezi la uhakiki wa ushindi wa mdemocrat Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba 3.

Mawakili wa Trump wataanza utetezi wao leo Ijumaa, wakihoji kwamba rais huyo wa zamani hawezi kuwajibishwa binafsi kwa uvamizi wa bunge. Wamehoji pia kabla kwamba mashtaka hayo hayana msingi kikatiba kwa sababu Trump hivi sasa hayuko tena madarakani, inagwa hoja hiyo ilitupiliwa mbali na Seneti mapema wiki hii.

 

DW