Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linakutana leo kujadili mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika nchini Myanmar, wakati ulimwengu ukiendelea kulaani mapinduzi hayo.
Marekani imetishia kuiwekea tena vikwazo nchi hiyo baada ya jeshi kutwaa madaraka na kumkamata kiongozi wake Aung San Suu Kyi na washirika wake usiku wa kuamkia Jumatatu.
Chama cha Aung San Suu Kyi kimetoa wito wa kiongozi huyo kuachiwa huru na jeshi kutambua ushindi wake katika uchaguzi uliofanyika mwezi Novemba. Hadi sasa haijulikani mahali aliko kiongozi huyo ikiwa ni zaidi ya saa 24 baada ya kukamatwa kwake.
Jeshi limekabidhi madaraka kwa Jenerali Min Aung Hlaing na kutangaza hali ya dharura kwa muda wa mwaka mmoja.
Leo Jumanne mawasiliano ya simu na intaneti yamerejeshwa lakini maeneo mengi ambayo huwa na shughuli nyingi yamesalia kuwa kimya.