Baraza la seneti nchini Marekani limemuondolea mashataka rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump, ya kuchochea shambulio baya dhidi ya jengo la bunge, kufuatia vurugu zilizosababishwa na kushindwa kwake katika uchaguzi. 

Maseneta 57 walipiga kura ya kumtia hatiani rais huyo wa zamani huku 43 wakikataa mashtaka dhidi yake. Warepublican saba waliunagana na Wademocrat wote kumtia hatiani Trump, lakini idadi hiyo ilikuwa chini sana ya kihunzi cha theluthi mbili iliyohitajika.

Matokeo hayo yameacha migawiko isiyo na utatuzi nchini humo kuhusiana na siasa za Trump zilizosababisha shambulio baya zaidi la ndani dhidi ya mmoja ya mihimili mitatu ya demokrasia ya Marekani. 

Ingawa aliondolewa hatia kuhusu shitaka pekee la kuchochea uasi, kesi hii ilishuhudia idadi kubwa zaidi ya maseneta kuwahi kupiga kura kumtia hatiani rais wa chama chao kwa makosa makubwa na madogo.