Rais wa Marekani Joe Biden amesema hatua ya Baraza la Seneti ya kumuondolewa mashtaka rais wa zamani Donald Trump ya kuchochea vurugu kwenye majengo ya bunge ni jambo linalokumbusha kuwa demokrasia imedhoofika. 

Biden ameyasema hayo saa chache baada ya Baraza la Seneti kushindwa kupata theluthi mbili ya kura ili kumtia hatiani Trump, anayekuwa kiongozi wa kwanza wa Marekani kushtakiwa mara mbili mbele ya Bunge. 

Biden amesema mwenendo huo unaonesha jinsi demokrasia inavyochechemea na kuwatolea wito raia wa nchi hiyo kusimama kidete kulinda ukweli na kupinga aina zote za hadaa. 

Katika kura ya jana maseneta 57 ikiwemo 7 kutoka chama cha Trump cha Republican, walipiga kura ya kumtia hatiani rais huyo wa zamani huku 43 wakikataa mashtaka dhidi yake.