Na. Edward Kondela
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limewakamata watuhumiwa wawili wa utoroshaji wa mifugo maeneo ya mipakani.

Kwa mujibu wa taarifa aliyotoa jana (02.02.2021), Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Blasius Chatanda alisema kufuatia operesheni kubwa ya kitaifa iliyoanzishwa hivi karibuni, ambayo ililenga kudhibiti matukio ya wizi wa mifugo pamoja na usafirishaji wa mifugo nje ya nchi bila kufuata utaratibu, jeshi hilo limewakamata watuhumiwa hao na linaendelea kuwasaka watuhumiwa wengine.

“Kama mnavyofahamu mpaka wetu wa Horohoro ni miongoni mwa mipaka ambayo inaweza kutumika kupeleka mifugo nje ya nchi hususan nchi jirani ya Kenya lakini pia bahari yetu (Bahari ya Hindi) inaweza kutumiwa pia kuvusha mifugo kupeleka Tanzania visiwani, Comoro, Ushelisheli lakini pia Madagascar, kufuatia operesheni hiyo kali na kabambe huku kwetu kulikuwa na watuhumiwa Wilaya ya Mkinga, walikuwa watuhumiwa watatu kati ya hao watuhumiwa wawili tayari wamekamatwa na wameshaunganishwa na wenzao kule Arusha ili kuendelea na taratibu za kichunguzi na hatimaye wafikishwe mahakamani.” Alisema Kamishna Msaidizi Chatanda.

Aliongeza kuwa Mkoa wa Tanga ni kati ya mikoa yenye wafugaji wengi na kuwasihi wale wote wanaojihusisha na vitendo vya utoroshaji wa mifugo waache mara moja, kwa sababu mkono wa sheria hautawaacha salama na kwamba serikali iko makini kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuhakikisha vitendo hivyo vinakoma na kubainisha kuwa katika mpaka wa Horohoro kwa miaka mingi mifugo ilikuwa haivuki kwa kufuata utaratibu, kwa kuwa ilikuwa inapitishwa njia zisizo rasmi na kwenda kwenye soko la jirani la nchi ya Kenya hali ambayo ilifanya wafugaji kuuza mifugo kwa hasara na wengine kupoteza mifugo wakati wa kuvusha kwenda nchi ya jirani.

Aliongeza kuwa kufuatia uchunguzi uliofanywa na Jeshi la Polisi ilibainika wapokeaji wengi wa mifugo walikuwa mpakani na wengine wakiwa na madaraka kwenye maeneo wanayoishi na kufafanua kuwa endapo suala hilo likiendekezwa wanaohusika hawawezi kubaki salama, lazima wakumbane na mkono wa sheria na waliokuwa wanafikiria kuanza kutorosha mifugo kwenda nchi ya jirani waache mara moja.

Mwishoni mwa wiki Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki alifanya ziara ya kikazi ya siku mbili Mkoani Tanga, ambapo wakati akiwa na mazungumzo na mkuu wa mkoa huo Mhe. Martine Shigella pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo, Mhe. Ndaki aliagiza kukamatwa kwa watuhumiwa wa utororshaji wa mifugo na mazao ya mifugo katika Mkoa wa Tanga na kuupongeza Mkoa wa Tanga kwa jitihada mbalimbali wanazozichukua katika kudhibiti wizi wa mifugo na utoroshaji wa mifugo kwenda nchi za nje.

Waziri Ndaki alisema watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake tayari wanafahamika kwa majina na mahali wanapoishi kufuatia ripoti aliyopatiwa na Jeshi la Polisi nchini kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo.

Mwanzoni mwa wiki iliyopita, Jeshi la polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na vyombo vingine vya ulinzi na usalama lilitoa taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa watatu wa wizi na utoroshaji wa mifugo maeneo ya mipakani.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Salum Hamduni, alisema jeshi hilo liliwakamata watuhumiwa hao katika tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani humo kufuatia agizo alilolitoa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki la kukamatwa kwa watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake.

Kamanda Hamduni alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao watatu kunatokana na baada ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutangaza operesheni ya kudhibiti wizi na utororshaji wa mifugo maeneo ya mipakani ambapo zilipatikana taarifa za uwepo wa watu wanaojihusisha na wizi na utoroshaji wa mifugo katika Wilaya ya Ngorongoro.

Aliongeza kuwa upelelezi bado unaendelea kuhusiana na tukio hilo, mara utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Alitoa wito kwa wananchi kuepuka usumbufu kwa kuhakikisha wanafuata sheria za biashara ya usafirishaji wa mifugo kwani wasipofanya hivyo watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.  

Hivi karibuni Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki akiwa katika ofisi za wizara hiyo zilizopo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma wakati akiwasilishiwa ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani aliliagiza Jeshi la Polisi nchini Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo kuwakamata mara moja watuhumiwa 67 wa utoroshaji wa mifugo na mazao yake kwenda nchi za jirani.

Katika ripoti ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani, iliyowasilishwa na Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Julius Mjengi kwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki, imeeleza kuwa kabla ya tarehe 7 Novemba, 2020, mifugo iliyokuwa inatoka kwenye minada ya awali ya Handeni na Kilindi kuelekea nchini Kenya kupitia mpaka wa Horohoro haikuwa inafuata taratibu za forodha kama shehena nyingine.

Aidha, ripoti hiyo ilibainisha kuwa takwimu za daftari la mifugo katika mpaka wa Horohoro zinaonyesha idadi ya mifugo iliyopitishwa kuelekea nchini Kenya kwa kipindi cha miaka 17 kutoka mwaka 2003 hadi Novemba, 2020 ilikuwa ni ng’ombe 24,980 na Mbuzi na Kondoo 9,368 (sawa na wastani wa Ng’ombe 122 na Mbuzi/Kondoo 46 kwa mwezi).

Pia, imefafanua kuwa baada ya uchunguzi, ilionekana kuwa kati ya tarehe 7 Novemba, 2020 hadi tarehe 9 Desemba, 2020 (kipindi cha mwezi mmoja tu) jumla ya Ng’ombe 1,096 na Mbuzi na Kondoo 1,044 walipitishwa katika kituo cha Forodha kuelekea nchini Kenya, ambapo huo ni wastani wa idadi ya mifugo iliyopita mpakani ndani ya mwezi mmoja ukilinganisha na siku za nyuma.

Katika ripoti hiyo ya uchunguzi, kuhusu utoroshaji wa mifugo mipakani, imebaini pia viashiria vya udanganyifu wa kurekodi idadi sahihi ya mifugo inayokaguliwa kwenda Kenya hususan katika mpaka wa Hororohoro – Tanga.

Mwisho.