Afrika Kusini imesitisha kuanza utoaji chanjo ya Astra Zeneca na Oxford baada ya utafiti kuonesha chanjo hizo hazina ufanisi katika kuzuia magonjwa mepesi na ya wastani kutoka kwenye aina mpya ya virusi.

Afrika Kusini ilipokea dozi milioni moja ya AstraZeneca wiki iliyopita na ilitarajiwa kuanza zoezi la kuwachanja Wahudumu wa Afya mwezi huu. Matokeo ya awali yaashiria chanjo ya AstraZeneca inaweza isiwe na manufaa.

Matokeo ya utafiti mdogo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Mjini Johannesburg, yanaeleza kuwa chanjo ya AstraZeneca inatoa kinga kidogo dhidi ya aina mpya ya kirusi cha Corona.

Waziri wa Afya, Zweli Mkhize amesema chanjo ya AstraZeneca inaonekana kuwa na ufanisi dhidi ya virusi vya mwanzo lakini sio hivi vinavyojibadili na hivyo wanasitisha zoezi hilo kwa muda.