Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Leonard Chamuriho, ameiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Mara , kuhakikisha wanapunguza  gharama za miradi, hususani wanapofanya upembuzi yakinifu.


Alitoa agizo hilo akiwa katika ziara wilayani Bunda, akikagua ujenzi wa barabara ya Nyamuswa-Bunda-Kisorya yenye urefu wa kilometa 121.9, pamoja na kipande cha barabara ya lami kutoka Bulamba-Kisorya (kilometa 51).


Akiwa katika ukaguzi huo, Waziri Chamuriho alisema barabara ya Nansio, ambayo inaanzia Nyamuswa-Bunda hadi Kisorya ni muhimu kwa  wananchi wa Wilaya ya bunda, kwamba itafungua fursa nyingi ikiwamo usafirishaji wa mazao.


Naye Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili alimpongeza  mkandarasi  anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo na TANROADS kwa kazi nzuri walioifanya katika ujenzi wa barabara hiyo.


Bupilipili alisema: “Kasi ya ujenzi ilikuwa kubwa katika ujenzi wa barabara hii na imetoa  ajira kwa vijana wazawa wa  Wilaya ya Bunda na Mkoa wa Mara. Niwapongeze na niwapongeze TANROADS kwa kazi nzuri wanayoifanya katika Wilaya hii ya Bunda mjini”.


Kwa upende wake Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Mara, Mhandisi Mlima Ngaile, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo alisema mkataba ulisainiwa na makubaliano yalikuwa ya miaka miwili, ila kutokana na kasi ya mkandarasi aliahidi kumaliza kazi hiyo kabla ya muda uliopangwa.


“Thamani ya mkataba Sh.bilioni 46.5 na unasimamiwa na  kampuni ya wahandisi ya ushauri kutokea TANROADS na hadi kufikia sasa mkandarasi ameshaanza kazi mbalimbali ikiwamo kujenga nyumba ya msimamizi ambayo imefikia  asilimia 50 na amesafisha barabara kutoka Bunda kwenda Bulamba," alisema mhandisi Ngaile.