WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza Halmashauri zinazolima mkonge nchini pamoja na wakulima wakubwa wa mkonge watenge ekari 10 kwa akili ya kuanzisha vitalu vya kuzalisha miche ya mkonge ili kupunguza tatizo la upungufu wa mbegu.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Kilimo itenge fedha katika bajeti yake kwa ajili ya kituo cha TARI Mlingano ili kukiwezesha kupanua eneo la uzalishaji miche kwa kununua vitendea kazi yakiwemo matrekta.

Ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Januari 20, 2021) baada ya kukagua kitalu cha miche ya mkonge la TARI Mlingano lililopo wilayani Muheza, Tanga na kufungua zoezi la ugawaji wa miche kwa wakulima wa zao hilo.

Waziri Mkuu amesema ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa miche ya mkonge nchini kila halmashauri na wakulima wakubwa wanatakiwa watenge ekari 10 kwa ajili ya kuandaa vitalu vya miche ya mkonge na kugawa kwa wananchi kwenye maeneo yao.

Amesema kituo cha TARI Mlingano kinatakiwa kijikite katika kufanya  utafiti wa mbegu bora pamoja na dawa za kudhibiti magonjwa katika zao hilo na suala la uzalishaji wa mbegu lifanywe kwa ushirikiano katika ya kituo hicho na wadau wa zao hilo.

Kadhalika, alisema kuwa lengo la serikali ni kuhakikisha mpaka ifikapo mwakani kuwa na ongezeko la uzalishaji wa miche zaidi ya Milioni mbili ya sasa kwani mahitaji ni makubwa kwa sasa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Mlingano, Dkt Catherine Senkoro amesema hadi kufikia Januari, 2021 jumla ya hekta 32.6 sawa na ekari 81.5 zimepandwa miche ya mkonge katika maeneo ya TARI Mlingano.

Amesema kituo chao kwa kushirikiana na Bodi ya Mkonge Tanzania imetoa mafunzo kwa wakulima na Maafisa Ugani katika baadhi ya mikoa inayofaa kwa kilimo cha mkonge ambayo ni Tanga, Morogoro, Pwani, Kilimanjaro, Lindi, Simiyu, Shinyanga na Mara. “Kufikia Desemba 2020, wakulima 422 na Maafisa Ugani 840 katika mikoa hiyo walipatiwa mafunzo.”

Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara ya Kilimo kupitia kituo cha TARI Mlingano imepanga kuzalisha miche 4,000,000 katika vitalu vyake, pia itapanua maabara ya uzalishaji wa miche kwa njia ya chupa  ili kuongeza kasi ya upatikanaji wa miche. Utaratibu huo unakadiriwa kuchangia miche milioni 10 kwa mwaka.

 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU