WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameendesha harambee ya papo kwa papo na kuchangisha sh. milioni 18.9 ambapo kati ya hizo, sh. milioni 10 zimetolewa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

“Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli anafuatilia tukio hili na amesema anamchangia Miriam shilingi milioni 10 ili ziweze kumsaidia katika mtaji wa biashara na umaliziaji wa ujenzi wa vyumba vya kupangisha”

Fedha hiyo ilichangishwa kwa ajili ya Miriam Msagati, binti mwenye ulemavu wa mwili ili ziweze kumsaidia kama mtaji wa biashara na uendelezaji wa ujenzi wa vyumba vya kupangisha katika nyumba ambayo amekabidhiwa leo (Ijumaa, Januari 22, 2021) na Waziri Mkuu. Gharama ya ujenzi wa nyumba na samani zilizomo ndani ni sh. milioni 47.32.

Waziri Mkuu ameendesha harambee hiyo kwenye kitongoji cha Fune, kata ya Mombo wilayani Korogwe baada ya kumkabidhi binti huyo nyumba aliyojengewa na wadau mbalimbali kutokana na mchango ulioasisiwa na Waziri Mkuu Machi 5, 2020 alipomtembelea Miriam na kumpatia mchango wa sh. milioni 5 za kuanza ujenzi wa nyumba hiyo.

Waziri Mkuu alimsaidia Miriam baada ya kumsikia binti akimuomba amsaide kupata makazi yeye na bibi yake kupitia kipindi cha Wape Nafasi kinachoongozwa na Tuma Dandi, mtangazaji wa Shirika la Utangazi Tanzania (TBC1).

Baada ya Waziri Mkuu kukabidhi nyumba hiyo, aliwaomba wadau wamchangie Miriam fedha ili apate mtaji pamoja na umaliziaji wa vyumba vya kupangisha ili aweze kujitegemea.

Akiwa bado anaendesha harambee hiyo, Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan alizungumza na wananchi hao kupitia simu aliyompigia Waziri Mkuu, ambapo alimpongeza kwa kuhakikisha Miriam anapata makazi bora. “Nimeona kazi kubwa iliyofanyika hapo, hongereni sana Waziri Mkuu pamoja na uongozi wa mkoa wa Tanga nami namuongezea shilingi milioni tano afanye mtaji.”

Kwa upande wake, Miriam baada ya kukabidhiwa nyumba hiyo alimshukuru Rais Dkt. Magufuli, Makamu wa Rais Mama Samia, Waziri Mkuu kwa uongozi wao wenye kujali wanyonge.

Alisema Tanzania imepata kiongozi mzuri anayewajali wanyonge, hivyo ameahidi kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awazidishie baraka ili wapate mafanikio mazuri zaidi.

“Siwezi kusahau kitu kama hiki, Mwenyezi Mungu ameniona, Mwenyezi Mungu awabariki watu wote walioshiki katika kufanikisha jambo hili kwani mmeweka hazina yenu kwa Mungu.”

Kwa upande wake, Muandaaji wa Kipindi cah Wape Nafasi, Tuma Dandi alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna inavyoshughulikia masuala mbalimbali ya watu wenye mahitaji maalumu.

“Nimeishiwa maneno, leo ni siku nyingine ambayo itaingia katika historia ya maisha yangu. Ninamshukuru Mwenyezi Mungu na Serikali kwa kufanikisha jambo hili kwani watu wenye ulemavu ni sehemu ya Watanzania ambao wanapaswa kuishi kama wengine.”

(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,