Na.Faustine Gimu Galafoni Dodoma.
Waziri wa Maji Jumaa aweso  Januari ,21,2021 ametembelea katika mradi wa ujenzi wa tenki  la  kuhifadhia maji  Buigiri Wilayani Chamwino mkoani Dodoma na kumwagiza meneja ufundi na Usanifu Mamlaka ya maji Safi na Usafi wa mazingira[DUWASA] Mhandisi Kashilimu Mayunga  kuisimamia vyema kampuni ya SUMA JKT inayotekeleza mradi huo kuongeza nguvu  kazi ili ukamilike kwa wakati.

Waziri Aweso  amesema kuna mpango wa uchimbaji wa visima 10 katika jiji la Dodoma na vilivyokamilika saba  ambapo visima hivyo vitakapokamilika vitaongeza lita milioni 21 hivyo ameiagiza DUWASA   kusimamia JKT ili mradi huo ukamilike kwa wakati ndani ya siku 60.

“Ni lazima tuongeze juhudi ya kuongeza huduma ya maji katika jiji la Dodoma,kubwa ambalo nakutaka Msimamizi acha kurukaruka tunataka tuone kazi inafanyika usiku na mchana”amesema.

Aidha,Waziri Aweso amesema Wizara haitakuwa kikwazo katika utekelezaji wa miradi  ya Maji  ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora ya maji na mpango wa sasa wa Wizara  ni kutekeleza mradi mkubwa wa Maji kutoka ziwa Victoria hadi Dodoma.

“Sisi kama wizara hatuna kikwazo katika utekelezaji wa miradi ya maji hivyo niwatake mnaosimamia mradi huu mfanye kwa juhudi kubwa”amesema .

Pia,Waziri Aweso ameitaka DUWASA kuwa  na usawa kila eneo  pindi inapofanya  mgao wa maji ili kuondoa manung’uniko kwa wananchi .

Katibu mkuu wizara ya Maji Mhandisi Athony Sanga amesema Mpango wa sasa kwa Wizara ni kufanya ziara za kushtukiza mara kwa mara katika miradi miradi ya maji ili kupata uhalisia huku Mwenyekiti wa Bodi DUWASA Prof.Davis Mwamfupe akisema kuwa wapo bega  kwa bega katika kutekeleza maagizo ya Wizara.

 Meneja ufundi na Usanifu Mamlaka ya maji Safi na Usafi wa mazingira[DUWASA] Mhandisi Kashilimu Mayunga  amesema tenki hilo lina uwezo wa ujazo wa lita milioni 2.5  ,gharama ikiwa ni milioni 998  huku  mbunge wa jimbo la Dodoma mjini Anthony Mavunde akiunga mkono juhudi  za serikali  ambapo Mkuu  wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamoga akiahidi kutoa ushirikiano wa taarifa juu ya mwenendo wa miradi ya maji.

Kapten..Deogratius  John Kaboya ni Meneja wa  SUMA JKT kanda ya kati Dodoma  ameomba upatikanaji wa vifaa vya kutosha katika kutekeleza ujenzi huo.

Ziara ya Waziri wa Maji imefanyika katika miradi miwili ya Maji ikiwemo tenki la Buigiri Chamwino pamoja na mradi wa kisima cha Ihumwa  lengo ni katika kuhakikisha tatizo la uhaba wa maji katika jiji la Dodoma linakuwa historia.

MWISHO.