Wakamatwa Kwa Madai Ya Wizi Wa Fedha Kwa Njia Ya Simu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Ialla jijini Dar es Salaam linawashikilia watu 10 kwa tuhuma za wizi wa mtandaoni na utapeli.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa Ilala, Janeth Magomi imeeleza kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa katika tarehe tofauti ya mwezi Januari mwaka huu katika maeneo tofauti ya Jiji la Dar es Salaam na wilayani Mkuranga mkoani Pwani.
Aidha, Mgomi ameeleza kuwa watuhumiwa hao wamekamatwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya wananchi kadhaa kutapeliwa fedha zao. Wananchi hao walitoa taarifa kwa jeshi hilo ndipo ukafanyika msako pamoja na kuweka mtego wa kubaini mtandao wa watuhumiwa hao.
Kufuatia tukio hilo Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala limewatahadhariasha watumiaji wa huduma za mitandao kuwa makini na watu ambao mara nyingi wanajifanya ni watoa huduma za mitandao husika na kuwalaghai wananchi ili kuwaibia.
Miongoni mwa watuhumiwa waliotiwa mbaroni ni pamoja na Baraka Makwaya, Fatuma Ayoub, Teddy Njauz, Modesta Njauz pamoja na Gift Makwaya.