Na. Catherine Sungura,WAMJW-Dodoma

Wizara ya Afya ipo tayari kupokea kero na malalamiko ya wananchi endapo itaonekana wameshindwa kusikilizwa ama kusaidiwa na viongozi wao wa ngazi za chini na wale wa vituo vya kutolea huduma za afya kwenye maeneo yao.

Hayo yameelezwa leo na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Abel Makubi mara baada ya kufanya kikao na Viongozi wakuu wa sekta ya afya kwa njia ya mtandao”ZOOM” kilichowajumuisha Waganga wakuu wa Mikoa na Wilaya,Wajumbe wa kamati ya usismizi wa huduma za afya za mikoa(RHMT) na wilaya (CHMT) pamoja na Wakurgenzi wa hospitali za Taifa,Kanda na Maalumu.

Prof. Makubi amesema kuwa wananchi wana matumaini na Serikali yao hivyo wanayo haki ya kusikilizwa na kutatuliwa kero zao kutoka kwa watendaji kwenye vituo vyote vya huduma za afya nchini hivyo kamati zote zinapaswa kufanya tathimini za kero zote kwa muda wa wiki nne na kuzitatua pia kuwasilisha ripoti Wizarani pamoja na TAMISEMI .

“Tunaanzisha utaratibu ambao sisi viongozi wa sekta ya afya tunaenda kutafuta kero kutoka kwa wananchi na kuzitatua,Hili ni agizo na tumekubaliana wasambae kwenye ngazi zote kuanzia zahanati,vituo vya afya na kwenye hospitali,tunatakiwa kuhakikisha wananchi wapate huduma bora licha ya kuwa tumeboresha huduma kwenye vituo vyetu”.

Aidha, amesema utaratibu huu utaweza kurahisisha kutatua kero za wananchi na kuweza kupunguza kero hizo na zingine sio lazima zimfikie Mhe. Waziri hivyo kama watendaji wanatakiwa kujitafakari wanaweza kutatua vipi changamoto wazipatazo wananchi.

“tumekubalikia suala la kuimarisha suala la uongozi, uwajibikaji na usimamizi kwani kila mmoja ameona kuna mapungufu kwenye usimamizi wa huduma za afya nchini,hivyo tumekubaliana kila kiongozi kuanzia Taifa hadi vijijini kusimamia sehemu zenye mapungufu kwani wananchi wanahitaji mazuri kutoka kwetu,hatuwezi kuwaridhisha kwa kila kitu lakini tutapunguza matatizo yao.

Upande wa kuimarisha vitengo vya huduma kwa wateja, Mganga Mkuu huyo wa Serikali amesema kitengo hicho kinatakiwa kuboreshwa na hivyo wanapaswa kuchakata kero zote na kuzifanyia kazi na hivyo kuzibandika kwenye ubao wa matangazo wa vituo vyao pia wanapaswa kuwa hai wakati wote kwakuwa mwananchi wanataka huduma za afya jinsi wanavyohitaji.

“Viongozi hao pia wanatakiwa kukagua ndani ya hospitali zao kwenye maeneo ya kutolea dawa na stoo kuona kama dawa zipo na zinawatosheleza wananchi,kama kuna wizi tuweze kuchukua hatu,waende kwenye wodi na OPD kuwasalimu wagonjwa na kama wana kero waseme ili wazitatue,pia maabara kuweza kuona kama vipimo vinafanyika”.Alisisitiza
Hata hivyo wamekubaliana kuwepo na magroup ya ‘Whatsap’ ambayo watapokea na kushughulikia kero kwenye kila wilaya au mkoa husika ili kila mwananchi awezo kutoa kero zake.

“Tumeagiza kuwe na namba ambazo zitatangazwa kwa wananchi,pia wawashirikie wananchi kupitia mikutano na kutaja namba zao ili wananchi wajue wanawasilisha vipi malalamiko yao ”.

Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kujenga imani na kuwaamini watendaji wote wa sekta ya afya, na kusema kuwa baada ya Mhe. Waziri kutangaza namba yake ya malalamiko kwa muda wa wiki mbili ameweza kupokea kero elfu tatu kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kikao hicho kwa njia ya mtandao kimehudhuriwa na washiriki wapatao 220 na ajenda kubwa ilikuwa ni jinsi ya kupunguza kero za wananchi zinazousiana na huduma za afya nchini ambazo wanatuma kupitia namba ya malalamiko iliyotangazwa na Waziri wa afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima mwishoni mwa mwaka jana ambayo ni 0734124191.
-MWISHO-