Msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo, ameishutumu Marekani kwa kujaribu "kupindua matokeo ya uchaguzi", kwa mujibu wa chombo cha habari cha Reuters.
Balozi wa Marekani nchini Uganda Natalie Brown Jumatatu alizuiwa kumtembelea kiongozi wa upinzani, Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, nyumbani kwake mjini Kampala.
"Kile ambacho amejaribu kufanya wazi kabisa, ni kuingilia siasa za ndani za Uganda, hasa uchaguzi, kubadilisha matokeo ya uchaguzi na mapenzi ya watu," Bwana Opondo amezungumza na shirika la Reuters.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani Jumatatu ilitoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi "wenye kujitegemea, wa uhakika, usiopendelea upande wowote, na wa kina" juu ya taarifa nyingi za uhakika" kuhusu wizi wa kura katika uchaguzi wa Uganda uliofanyika wiki iliyopita.
Rais Yoweri Museveni, aliyeshinda uchaguzi kwa awamu ya sita, amekanusha madai ya wizi wa kura.