Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema serikali yake imefungia mitandao ya kijamii nchini humo kuelekea uchaguzi wa rais ambao umepangwa kufanyika kesho Alhamisi.

Museveni aliyezungumza usiku wa kuamkia leo ameishutumu kampuni ya Facebook kwa kile alichokitaja kuwa ujeuri, baada ya kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii kufunga akaunti kadhaa zinazohusishwa na kampeni yake kutaka achaguliwe tena.

Museveni amesema ana uhakika serikali imefunga mitandao ya kijamii na amewaomba msamaha Waganda kwa hali hiyo.

Akizungumza kuhusu mtandao wa Facebook, Museveni amesema ikiwa mtandao wowote unataka kufanya kazi Uganda, basi ni lazima utoe nafasi sawa kwa wote, lakini ikiwa unataka kuwa na upendeleo dhidi ya chama tawala basi hauruhusiwi.

Hakukuwa na jibu au kauli ya moja kwa moja kutoka kwa kampuni ya Facebook kuhusu hatua hiyo ya Rais Museveni.

 

-DW