Matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais uliofanyika Alhamisi nchini Uganda yaliyotolewa usiku wa kuamkia leo yanaonesha rais Yoweri Museveni anaongoza dhidi ya mpinzani wake mkuu Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine.

Kulingana na Tume ya Uchaguzi nchini humo matokeo ya awali kutoka vituo visipungua 300 vya kupigia kura, yanaonesha rais Museveni wa Chama tawala cha NRM amepata asilimia 61.3 huku Bobi Wine wa Chama cha NUP akivuna asilimia 27.9 ya kura hadi sasa.

Hata hivyo bado ni mapema ikizingatiwa kuwa idadi ya vituo 300 ambako zoezi la kuhesabu kura limemalizika ni ndogo ikilinganishwa na zaidi ya vituo 34,000 vilivyotumika katika uchaguzi huo hapo jana.