Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ufaransa Jean-Yves Le Drian, amesema kukamatwa kwa maelfu ya watu nchini Urusi wakati wa maandamano ya kumuunga mkono mkosoaji wa serikali ya Urusi Alexei Navalny kunauweka mashakani utawala wa sheria. 

Le Drian ametaka vikwazo dhidi ya Urusi vitekelezwe huku akisema kupitia radio moja ya Ufaransa kwamba ana wasiwasi wa taifa hilo kuingia katika utawala wa kimabavu. 

Polisi nchini humo imewakamata zaidi ya watu 3000 hapo jana katika maandamano yaliohudhuriwa na maelfu ya watu. 

Kwa sasa waendesha mashitaka wa Urusi wanachunguza uwezekano wa polisi kuhusika katika ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya waandamanaji, waliomiminika mitaani kufuatia wito uliotolewa na Navalny wa maandamano dhidi ya utawala wa Rais Vladimir Putin. 

Alexei Navalny alikamatwa katika uwanja wa ndege wa Moscow alipokuwa anarajea nchini kutoka Ujerumani alikokuwa anapata matibabu baada ya kisa cha jaribio la kuuawa kwa kupewa sumu Agosti mwaka uliopita.