Rais wa Uganda,
Yoweri Kaguta Museveni, ameamua kumteua Brigedia Kayanja Muhanga, kusimamia masuala ya usalama wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo unaotarajiwa kufanyika tarehe 14 Januari 2021.
 

Uteuzi ho unampa nafasi Brig. Muhanga kuratibu vikosi vyote vya usalama nchini humo ambavyo vitasubiri sauti yake katika utekelezaji wa jambo lolote.

Luteni Deo Akiiki ambaye ni Naibu Msemaji wa Jeshi la Uganda amesema, Brig. Muhanga atakuwa mratibu wa operesheni za vitengo vyote ikiwa ni pamoja na vikosi vya polisi, jeshi na idara ya ujasusi na usalama.

‘Ni kweli kwamba, Brigedia Kayanja Muhanga amepewa nafasi ya kuratibu vikundi vyote vya usalama kwa madhumuni ya kuunganisha shughuli ya usalama wa pamoja hususan katika Mji wa Kampala na nchi yote,’ amenukuliwa Luten Akiiki.

Kuelekea uchaguzi mkuu nchini humo, Tarehe 17 Desemba 2020, Rais Museveni alimteuwa mwanaye Luteni Jenerali Muhoozi Kainerugaba kuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi wa Rais (SFC).

Jenerali Muhoozi, ni mtoto wa kwanza wa rais huyo ambaye amekuwa madarakani kwa miongo minne sasa.

Kabla ya uteuzi huo, Jenerali Muhoozi, alikuwa mshauri wa baba yake – Rais Museveni – katika masuala ya ulinzi.