Mtandao wa kijamii wa Twitter umeifungia moja kwa moja akaunti ya Rais wa Marekani Donald Trump hapo jana Ijumaa, ikitoa tahadhari ya uchochezi wa vurugu zaidi.

Kwa muda mrefu mtandao wa Twitter umempatia kinga Rais Trump na viongozi wengine wa ulimwengu katika sheria zake, dhidi ya mashambulizi binafsi, matamshi ya chuki na tabia nyingine ambazo ni kinyume na maadili.

Lakini katika maelezo ya kina yaliyowekwa kwenye blogi ya mtandao huo Jana Ijumaa, kampuni hiyo ilisema taarifa za hivi karibuni za Trump zilionyesha kuhimiza vurugu zilizozuka katika majengo ya bunge, na kuashiria mipango inayozunguka mtandaoni ya maandamano ya kujihami kwa silaha wakati wa maandalizi ya kuapishwa kwa Rais mteule Joe Biden.

Hata hivyo Trump amesema kupigwa marufuku kutumia mtandao huo ni kubinya uhuru wa kujieleza. Kupitia akaunti ya Serikali ya Marekani, Trump ameandika kuwa kampuni hiyo inajaribu kumnyamazisha.

 Credit: DW