Rais wa Marekani Donald Trump anayeondoka madarakani ametoa hotuba yake ya mwisho kuwaaga Wamarekani huku akisema, walifanya kile walichokuja kufanya na walipata mafanikio makubwa.

Katika hotuba yake, Trump hakumtaja Biden kama mshindi wa uchaguzi uliopita, lakini alitumia dakika 20 za hotuba yake kuelezea mafaniko ya uongozi wake.

‘Tulirejesha nguvu ya Marekani nyumbani na nje ya nchi, dunia inatuheshimu tena, tulijenga uchumi imara katika historia ya dunia hii, tuliimarisha mahusiano yetu nje ya nchi hasa dhidi ya China,’

‘Lakini tumesababisha uwiano katika eneo la mashariki ya kati, hakuna aliyeamini na sasa eneo hilo lina mwamko mpya, najivunia kuwa rais wa kwanza kwa muda mrefu  ambaye  hakuanza vita vipya ,’ alisema Trump.

Saa chache kabla ya kuondoka kwake, Trump ametoa msamaha kwa wanamuziki Lil Wayne na Kodak Black  na aliyekuwa Meya wa mji wa Detroit Kwame Kilpatrick huku aliyewahi kuwa mshauri wake Steve Bannon, akitarajiwa pia kusamehewa.

Katika hatua nyingine, idadi ya watu waliopoteza maisha nchini Marekani kutokana na janga la Corona, sasa imeongezeka na kufikia zaidi ya 400,000 kwa mujibu wa takwimu za chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Saa chache kabla ya kuapishwa kwake, rais mteule Joe Biden amewakumbuka Wamarekani waliopoteza maisha kutokana na janga hilo.