Tozo Za Masoko Ya Samaki Ya Kimataifa Kuwasilishwa Wizarani
Na. Edward Kondela
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amewataka wakurugenzi wa halmashauri zenye masoko ya samaki ya kimataifa kuacha kupanga tozo za mazao ya uvuvi bila kuwasiliana na wizara hiyo ili kuondoa kero za tozo zinazowakumba wananchi wanaofanya biashara katika maeneo hayo.
Akizungumza jana (03.01.2021) mara baada ya kutembelea mnada wa mifugo uliyopo Kijiji cha Buzirayombo Kata ya Bukome na soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya Muganza, Wilaya ya Chato Mkoani Geita, Waziri Ndaki amesema wizara haitaki kusikia kero za wafanyabiashara kuhusu tozo zisizo rafiki katika masoko hayo likiwemo soko la samaki la kimataifa la Kata ya Kirumba lililopo Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza.
“Kuhusiana na tozo niseme tu kwa wakurugenzi walio na masoko haya ya kimataifa kwa maana ya soko la Kirumba na Kasenda, sisi wizara hatutaki kusikia kelele katika haya masoko mnapopanga tozo zenu hakikisheni kwa masoko haya mawili tuwasiliane ili tupange tozo za kwenu na kwetu ambazo zitakuwa rafiki.” Amesema Mhe. Ndaki
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani amemuomba Waziri Ndaki kupitia vikundi vya wavuvi vilivyosajiliwa, wizara ione namna ya kuwasaidia wavuvi mikopo yenye riba nafuu pamoja na kuwanunulia nyavu ili kuacha kujihusha na uvuvi usiofuata utaratibu.
Nao baadhi ya wavuvi na wananchi wanaofanya shughuli za kibiashara katika soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda wamesema wanashirikiana na serikali kuhakikisha wanadhibiti uvuvi haramu.
Aidha, wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi namna inavyofanya jitihada za kuhakikisha inaboresha mazingira ya wavuvi ili sekta ya uvuvi iweze kuwa na tija kwa wadau wa sekta hiyo na hatimaye waweze kunufaika kiuchumi.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amekagua pia ujenzi wa machinjio ya kisasa yanayojengwa katika eneo la mnada wa mifugo Kijiji cha Buzirayombo Kata ya Bukome, Wilaya ya Chato Mkoani Geita.