Taarifa Ya Kukamatwa Kwa Waethiopia 61 Kwa Kosa La Kuingia Nchini Bila Kibali.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwakamata Waethiopia 61 kwa kosa la kuingia nchini bila kufuata taratibu za nchi.
Ni kwamba tarehe 12.01.2021 majira ya saa 23:00 usiku huko Kijiji cha Gari Jembe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Askari Polisi wakiwa kazini katika kizuizi [Barrier] kilichopo barabara kuu ya Mbeya – Tukuyu walilisimamisha Gari yenye namba za usajili T.509 AZZ Scania Lori lililokuwa likiendeshwa na dereva RABDI RAMADHANI [48] Mkazi wa Unga Limited Arusha.
Askari walianza kufanya ukaguzi kwenye Gari hilo na kumtaka dereva kufungua mlango wa nyuma ya Gari hilo na ndipo walimkamata DAWAT TADESA [22] Raia na Mkazi wa nchini Ethiopia akiwa na wenzake 60 kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.
Awali katika mahojiano, dereva wa Gari hilo alidai kuwa amepakia bidhaa mbalimbali za dukani lakini baada ya kuamriwa kufungua mlango wa nyuma wa Gari hilo ndipo ilibainika amepakia/anasafirisha wahamiaji haramu kuelekea Kasumulu mpaka wa Tanzania na Malawi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, tunaendelea na mahojiano dhidi ya mtuhumiwa RABDI RAMADHANI [48] Dereva aliyekuwa akisafirisha wahamiaji hao ili kubaini mtandao mzima wa mawakala wa kusafirisha wahamiaji.
Mtakumbuka Oktoba 22, 2020 huko Wilaya ya Mbarali, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata Waethiopia 22 kwa kosa la kuingia nchini bila kibali. Sambamba na hilo Disemba 15, 2020 huko Wilaya ya Rungwe Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Maafisa wa Idara ya Uhamiaji lilifanikiwa kuwakamata Waethiopia 57 kwa kosa la kuingia nchini bila kibali pamoja na mawakala wawili waliokuwa wakiwasafirisha.
WITO WA KAIMU KAMANDA:
Ninatoa wito kwa wasafirishaji wa wahamiaji haramu nchini kujiepusha kufanya biashara haramu ya binadamu kwani ni kinyume cha sheria za kimataifa na hata maadili na dini pia inakatazwa.
Kwamba wanaojihusisha na biashara hiyo haramu wajue kwamba kusafirisha wahamiaji haramu ni kosa la jinai lenye adhabu kali na vyombo vinavyotumika kuwasafirishia hutaifishwa kwa amri ya Mahakama.
Kwamba Mbeya hapapenyeki na iwapo utajaribu tu biashara hiyo haramu utaishia mkononi mwa vyombo vya dola kwani tumejipanga vilivyo kuzuia na kupambana na uhalifu na wahalifu wa kila aina.