Sheria Itumike Kuwabana Wanaohujumu Miundombinu Ya Barabara
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, ameitaka Bodi ya mfuko wa Barabara (RfB) kutumia vifungu vya sheria vitakavyowabana watumiaji wa barabara wanaoegesha magari kwenye mabega ya barabara, wanaoiba alama za barabarani pamoja na wanaopitisha mifugo kwenye barabara.
Mhandisi Kasekenya ameyasema hayo, alipotembelea ofisi za Mfuko huo zilizoko Njedengwa, jijini Dodoma ili kujifunza shughuli zinazofanywa na mfuko huo.
“Simamieni sheria na muwachukulie hatua wale wote wanaoujumu miundombinu ya barabara kwa namna moja ama nyingine ili tuzilinde barabara zetu na kutotumia fedha nyingi katika matengenezo”. amesema Mhandisi Kasekenya.
Aidha, amewataka Mameneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha wanaziba mashimo barabarani ndani ya masaa 48 kama sheria inavyoelekeza ili kupunguza ajali zinazoweza kutokea kutokana na uwepo wa mashimo hayo.
“Hakikisheni mnakuwa na uwezo wa kupata taarifa kwa kuambiwa au kukagua ili kubaini mashimo yaliyopo barabarani na kuziba mashimo haya ndani ya masaa 48, Sheria itachukua mkondo wake kwa yeyote asiyetii sheria hii’’, amesisitiza Kasekenya.
Naye, Meneja wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Eliud Nyauhenga, pamoja na mambo mengine amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa Mfuko unafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kukusanya fedha, kugawa fedha kwa Taasisi husika pamoja na kufuatilia matumizi ya fedha hizo.
Aliongeza kuwa, asilimia 70 ya makusanyo inapelekwa kwenye ukarabati wa barabara za kitaifa ambazo ziko chini ya wakala wa Barabara nchini (TANROADS) na asilimia 30 inapelekwa kwenye ukarabati wa barabara zilizoko chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Nyauhenga, amefafanua kuwa mfuko huo unategemea vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo tozo za mafuta na barabara, tozo za magari ya kigeni (Transit fees) pamoja na tozo inayolipwa na wanaozidisha uzito wa magari barabarani.
Kasekenya, ametembelea Bodi ya Mfuko wa Barabara ambayo imekuwa ikitoa fedha kwa ajii ya matengenezo ya barabara nchini zinazosimamiwa na TANROADS pamoja na TARURA na kuhakikisha kuwa hali ya mtandao wa barabara nchini inakuwa bora.