Na. WAMJW-Tabora
Wizara ya Afya imeokoa takribani shilingi milioni 389 katika ujenzi wa jengo la Idara ya huduma za wagonjwa wa dharura linalojengwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tabora- Kitete ambalo limewekwa jiwe la msingi na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Hayo yameelezwa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia Dkt. John Pombe Magufuli alipokua akitoa salamu za wizara hiyo kwa wakazi wa mkoa wa Tabora.
Dkt. Gwajima alisema ujenzi wa jengo hilo litakalo wahudumia wakazi wa Tabora, mikoa ya jirani na hata nje ya nchi kutokana na barabara kuu zinazopita mkoani hapo kwakuwa jengo hilo litakua na uwezo kuwahudumia wagonjwa 50 hadi 60 tofauti na awali ambapo walikua wakihudumia wagonjwa 3 hadi 5.
Alitaja gharama za ujenzi wa jengo hilo ni milioni 604.3 ambao zimetolewa kwa ushirikiano na mfuko wa dunia (Global Fund) na ujenzi wake umetumia mfumo wa ‘force Account’ na hivyo limeweza kuokoa fedha hizo na endapo lisingetumia njia hiyo lingegharimu zaidi ya shilingi bilioni moja.
Vile vile Dkt. Gwajima alisema wamepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. Rais na kuahidi yeye na wizara yake kufanyia kazi ikiwemo kuongeza madaktari bingwa, kuwafuatilia wale walioondoka pamoja na jengo la huduma la mama na mtoto kwa ajili ya kujifungua na ICU.
Miradi mingine ya ujenzi wa Idara ya huduma za wagonjwa wa dharura nchini ambayo wizara inashirikiana na Global Fund inatekelezwa na ipo hatua mbalimbali za kukamilishwa katika mikoa ya Ruvuma, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Mara na Tanga.