Serikali imeingia makubaliano na wafanyabiashara ya zao la ngano kuwa wale wote waliokuwa wakiagiza ngano nje ya nchi sasa watanunua asilimia 60 ya ngano hiyo hapa nchini ili kukuza soko la wakulima na kuhakikisha nchi inajitosheleza.

 
Makubaliano hayo yameingiwa  tarehe 23 Januari, 2021 Jijini Dodoma kati ya Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda na Wafanyabiashara wakubwa wa ngano nchini yaliyoshuhudiwa na Wakulima wakubwa na wadogo wa ngano toka mikoa yote inayozalisha ngano nchini.

 
“Tumekubalina sisi Serikali na Wafanyabiashara kuwa wale wote wanaoingiza ngano toka nje sasa watainunua ngano hiyo kwa prolata ya asilimia 60 ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya nchi ili kutoa fursa ya Wakulima mwengi wakubwa na wadogo kupata soko hali itakayochangia kuongeza uzalishaji zaidi”. Alisema Prof. Mkenda.

 
Waziri huyo wa Kilimo alisema makubaliano hayo ya kuwa na bei ya Shilingi mia nane (800) kwa kilo ya ngano yanaweza kuwa na maumivu kidogo kwa Wafanyabiashara lakini wamekubalina kwa pamoja kuanzia hapo na kuwa ubora wa ngano utazingatiwa kwenye bei hiyo.

 
Katika kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Viongozi Wakuu wa Wizara, Wakuu wa mikoa ya Arusha na Manyara pamoja na Waagizaji Wakubwa wa ngano; Ikiwemo Kampuni ya Bakhresa Group Ltd, Azania, AMSONS, TBL, Sunkist na Jumbo wamekubaliana kuwa kuanzia sasa Kampuni hizo zitanunua kutoka kwa Wakulima kiwango kile kile na sawa na kiwango wanachonunua toka nje ya nchi kwa bei ya kuanzia Shilingi 800 kwa kilo.

 
Prof. Mkenda alitaja maeneo mengine ya makubaliano kuwa ni Wakulima wakubwa waliopewa mashamba ya Serikali; Wanatakiwa kulima ngano au shairi sasa vinginevyo Serikali itayachukua mashamba hayo na kugawa kwa Wawekezaji na Wakulima wadogo kwenye maeneo hayo.

 
Eneo jingine la ushirikiano walilokubaliana ni la kuhakikisha Serikali inasimamia ubora wa ngano inayozalishwa kwenye mashamba ili iendani na mahitaji ya soko ambapo  Waziri wa Kilimo Prof. Mkenda amesema tayari Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo nchini (ASA ) wamepewa jukumu hilo la kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mbegu pamoja na mahitaji ya viuatilifu na madawa.

 
Ili kuhakikisha Wizara inafanya kazi kwa karibu na wadau wa kilimo, Waziri Mkenda amesema wataanzisha Dawati Maalum la Sekta Binafsi ili litumike kama kiungo na wafanyabiashara kutatua changamoto za kibiashara kwenye mazao yote ya kikamkakati ikiwemo ngano na mengine.

 
“Tunaanzisha Dawati la Sekta Binafsi wizarani ili lisaidie kukuza biashara na kuondoa changamoto za upatikanaji masoko na huduma zingine muhimu kuwezesha Serikali na Wadau kutimiza malengo yao ya kuhudumia watanzania”. Alisema Prof. Mkenda.

 
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Makampuni ya Bakhresa Sufian Omary alisema kampuni ipo tayari kuanza kutekeleza makubaliano hayo na serikali ili mkakati wa kukuza uzalishaji wa ngano hapa nchini uweze kuwa na matokeo chanya na kunufaisha pande zote mbili.

 
Naye mwakilishi wa kampuni ya Azania Group Hafidh Mohamed alitoa pongezi kwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa kutaka kuona nchi inajitosheleza kwa uzalishaji wa ngano ndio maana wizara ya kilimo imeamua kukutana na wadau wa zao hilo.

 
Hafidhi alisema Kampuni ya Azania imeanzishwa kwa ajili ya Watanzania hivyo itahakikisha inakidhi mahitaji ya nchi na kuwa itatekeleza mkakati huu wa Serikali ili Wakulima wa zao la ngano wapate uhakika wa masoko ya mazao yao.

 
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa mikoa ninayolima ngano; Mkuu wa Mkoa wa Manyara Joseph Mkirikiti amewapongeza Waagizaji wakubwa wa ngano kwa kuitikia wito wa serikali na kukubali kuingia makubaliano ya kuanza kununua ngano ya Wakulima hatua itakayokuza uzalishaji na kuifanya nchi ijitosheleze kwani Tanzania ina ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo hicho.

 
Mkirikiti alibainisha kuwa zao la ngano lina fursa kubwa ya kukuza uchumi endapo uhakika wa soko la ndani utapatikana kwani wakulima wapo tayari kulima na pia akaonya wawekezaji ambao wanahodhi maeneo makubwa bila kulima ngano kuwa serikali itachukua hatua kali.

 
“Ipo kampuni ya Ngano Ltd wana maeneo makubwa zaidi ya ekeari 20,000 hawazitumii,nawasihi wakalime ngano vinginevyo tutachukua hatua za kuwanyanganya”. Alisema Mkirikiti.

 
Mkulima wa ngano toka Sumbawanga Bwana Msigwa akizungumza kwa niaba ya wakulima alisema uamzuzi wa serikali kuwakutanisha na wafanyabiashara wakubwa wa ngao umesaidia kupata uhakika wa masoko kwani miaka mingi walikatishwa tamaa kulima ngano.

 
Msigwa alisema amekuwa akilima ngano lakini changamoto yake ni soko hatua iliyosababisha kushindwa kurejesha mikopo ya biashara,hivyo makubaliano haya ya wizara ya  wadau wa ngano ni mwanzo mzuri wa kuwasaidia wakulima kupata soko.

 
“Tumekuwa tukikopa fedha tuaanzisha mashamba ya ngano lakini tunakosa soko leo ni faraja kuona tumehakikishiwa na wafanyabiashara watanunua ngano yetu. Asante sana kwa Serikali kufanikisha hili”. Alisema Bwana Msigwa.