Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Serikali itaweka mazingira wezeshi ya kuendeleza vijana wabunifu wa TEHAMA nchini

Ndkt. Ndugulile ameyasema hayo jana  wakati wa ziara yake ya kutembelea Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) na Ndaki ya TEHAMA ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (COICT) zilizopo Dar es Salaam

Amesema kuwa vijana wanabuni mifumo mbali mbali ya TEHAMA ya kutatua changamoto za wananchi ila wanakosa mazingira wezeshi ya kuendeleza na kukuza bunifu zao kama vile kupatiwa muda maalumu wa kuingiza sokoni bunifu zao kwa kufanya majaribio ya bunifu hizo kukubalika kwa wananchi bila kulazimika kulipia gharama za usajili, kupata masoko, malipo ya kodi na leseni kuendana na matakwa ya uendeshaji wa kampuni na biashara nchini

Amesisitiza kuwa azma ya Serikali ni kuendeleza wabunifu wa TEHAMA ili waweze kutengeneza mifumo kuendana na mahitaji ya wananchi badala ya kuendelea kununua mifumo hiyo kwa gharama kubwa kutoka nje ya nchi ambapo Serikali inatumia fedha nyingi kununua mifumo ya TEHAMA

Amefafanua kuwa utengenezaji wa mifumo ya TEHAMA hapa nchini utaongeza wigo wa matumizi ya intaneti na huduma za mawasiliano na itajibu changamoto za wananchi na ametoa rai kwa watanzania kujenga imani ya kutumia teknolojia rahisi zinazobuniwa na vijana wa ndani ya nchi bila kujali umri, uzoefu au majina ya kampuni zao

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu amesema kuwa vijana haom wameanzisha kampuni zaidi ya 20 za mifumo ya TEHAMA na tayari mifumo hiyo inasaidia kukusanya kodi kwenye halmashauri; kuwawezesha vijana kusoma VETA kwa njia ya mtandao na TIGO kuweza kuhifadhi taarifa za wateja wake

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu, utafiti na ubunifu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Benadetha Kiliani na Mkuu wa Ndaki ya TEHAMA ya Chuo hicho, Dkt. Mussa Kisaka wamesema kuwa Chuo kiko tayari kushirikiana na Wizara ili kuendeleza vijana wabunifu na watafiti wa TEHAMA nchini

Akizungumza kwa niaba ya vijana wabunifu wa TEHAMA, Geofrey Magila ameiomba Serikali kuwawezesha wakubalike na kuaminika na wapewe kazi badala ya kampuni zao kufanya kazi kwa kutumia mgongo na majina ya kampuni nyingine kwa kuwa kampuni zao ni changa na hazina mtaji wa kutosha kuingia kwenye ushindani wa zabuni zinazotangazwa zinazohusu mifumo ya TEHAMA

“Tulipata kazi kutoka kampuni ya AIS ya simu za mkononi ya Malyasia yenye wateja zaidi ya milioni 50 ambao walituamini na tuliwatengenezea mifumo ya kulinda taarifa za wateja wao, ndipo baadae baadhi ya kampuni za ndani ya nchi zikaanza kutuamini,” amesema Magila

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari