Waziri wa Viwanda na Biashara, Geofrey Mwambe amewaonya wafanyabiashara wa mafuta ya kula watakaopandisha bei ya bidhaa hiyo kinyume na bei elekeze kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo kufutiwa leseni zao za biashara.

Waziri Mwambe ametoa onyo hilo jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa habari juu ya mfumuko wa bei ya mafuta ambao umekua mkubwa kwa siku za  hivi karibuni.

“Kwa sasa changamoto ya bei haitakuwepo na tayari tumeshawapunguzia waagizaji baadhi ya gharama za kushusha mafuta pale bandarini lakini pia niwahakikishie watanzania uhaba wa mafuta hauwezi kuendelea kwani Februari 17 kuna meli ya mafuta itawasili na nimeagiza isichukue muda mrefu kushusha pale bandarini hadi Februari 20 meli hiyo iwe imeshashusha mafuta” amesema.

Amewataka watanzania hususa ni vijana kuchukulia changamoto ya uzalishaji wa mafuta nchini kuwa ni fursa kutokana na kuwa na ardhi inayokubali mazao ya mafuta amesema ni wajibu kwa wakulima kulima kwa wingi mazao hayo.

Aidha waziri Mwambe ametoa maelekezo kwa Tume ya Ushindani kuhakikisha wanafuafitilia mwenendo wa mafuta nchini huku akiwataka kumuandalia ripoti ya hali ya bidhaa hiyo hapa nchini nchini.

Amewataka Wakuu wa Mikoa ambao mikoa yao ina ardhi inayokubali mazao ya mafuta kama michikichi, alizeti na karanga na mazao mengine ya mafuta kuhamasisha Wananchi wao kujikita kwenye kilimo hicho ili kuweza kujikwamua kiuchumi wao wenyewe lakini pia kuzalisha mbegu ambazo zitatumika na viwanda vya ndani na kupunguza  uagizwaji wa mafuta nje ya Nchi.