RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imedhamiria kuendeleza amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Zanzibar ambayo inakwenda  sambamba na misingi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere.


Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na uongozi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere ukiongozwa na Mkurugenzi  wake Joseph Butiku uliofika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza kwa kuchaguliwa kwua Rais wa Zanzibar pamoja na kuendeleza Serikali ya Umoja wa Kitaifa.


Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa  kuwepo kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa imeweza kuimarisha amani, umoja na mshikamano hapa Zanzibar  hatua ambayo ni chachu ya maendeleo na imekuwa ikisisitizwa siku zote na Taasisi ya Mwalimu Nyerere.


Alisema kuwa hivi sasa kumekuwepo maelewano na mashirikiano makubwa kati ya viongozi pamoja na wananchi walio wengi wa Zanzibar hali ambayo imepelekea kuimarika kwa umoja, amani na mshikamano tokea kumalizika kwa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hapa nchini.


Aliongeza kuwa hatua hiyo imefikiwa kutokana na maridhiano yaliyofanyika ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo lengo na madhumuni yake makubwa ni kuendeleza umoja, amani na mshikamano ili Zanzibar izidi kupata maendeleo na wananchi wake wazidi kuelewana.