Na Nelson Kessy, Chato
Rais wa Jamhuri ya Msumbiji,  Mhe. Filipe Jacinto Nyusi anatarajia kufanya ziara ya kikazi ya siku mbili hapa nchini Tanzania kuanzia tarehe 11 - 12 Januari 2021 kwa mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Akithibitisha juu ya ziara hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amesema kuwa Mhe. Nyusi atawasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na kupokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika uwanja wa ndege wa Geita - Chato.

"Ziara hii ya Rais Nyusi ni ziara ya kindugu ambayo ilipangwa kufanyika muda mrefu lakini haikuweza kufanyika mapema, kutokana na kutokana na sababu mbalimbali, hususan Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika Oktoba 28, 2020," Amesema Prof. Kabudi.

Aidha, Prof. Kabudi ameongeza kuwa, ziara ya Mhe Nyusi, ni kwa ajili ya kuendeleza na kuimarisha mahusiano ya nchi zetu mbili katika maeneo anuwai, yakiwemo yale ya kidiplomasia, kiuchumi, kisiasa na kijamii; kama yalivyoasisiwa na vyama vya ukombozi vya nchi zetu, yaani, chama cha TANU na Chama cha Afro-Shirazi na baadaye Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa upande wa Tanzania na kile cha FRELIMO kwa upande wa Msumbiji. Mtakumbuka, mahusiano haya yaliyotukuka, yaliasisiwa na viongozi waanzilishi wa nchi zetu huru, yaani Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa upande wa Tanzania na Hayati Dkt. Eduardo Tshivambo Mondlane kwa upande wa Msumbiji.

"Uhusiano huo pia umeendelea baada ya Msumbiji kupata uhuru wake kupitia mapambano ya silaha mwaka 1975, ambapo, kama nyote mnavyofahamu, kuanzia Rais wa Kwanza wa Msumbiji Huru, Hayati Samora Moises Machel, na wengine wote waliomfuatia hadi leo, na Marais wa Tanzania baada ya Hayati Baba wa Taifa hadi leo, wote wameendelea kuimarisha mahusiano hayo na undugu wa Watanzania na Watu wa Msumbiji ambao kwa hakika ni ndugu wa damu," Ameongeza Prof. Kabudi

Prof. Kabudi ameeleza kuwa, licha ya uhusiano wa Kihistoria na Kidiplomasia kati ya nchi zetu mbili, uhusiano wa Kiuchumi nao umeendelea kuimarika. Tanzania inafanya biashara na Msumbiji kupitia mazao ya chakula na biashara pamoja na bidhaa za viwandani. Kwa mfano, takwimu kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zinaonesha kuwa jumla ya mauzo ya Nje (Export) kati ya nchi hizi mbili zilifikia Shilingi za Kitanzania Bilioni 76.4 kwa mwaka 2018 na Shilingi za Tanzania Bilioni 93.5 kwa mwaka 2019.

Kuhusu uwekezaji, hadi sasa makampuni makubwa ya Kitanzania yaliyowekeza mitaji mikubwa nchini Msumbiji ni pamoja Bakheresa (Azam), Mohammed Enterprises, Quality Foam (Magodoro Dodoma), n.k. Vilevile kuna Watanzania wanaomiliki kampuni za usafirishaji wa abiria na mizigo pamoja na biashara za kati na ndogondogo nchini Msumbiji.

"Licha ya changamoto ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID 19) SADC imeendelea kuwezesha na kusimamia biashara miongoni mwa nchi wanachama. Wakati wa ziara hii viongozi wetu watabadilishana mawazo ya namna ya kuendelea kuwezesha ufanyaji wa biashara," Ameongeza Prof. Kabudi

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Luhumbi amewataka wananchi wa Geita kujitokeza kwa wingi na kumpokea mgeni wakati atakapokuwa amewasili katika uwanja wa ndege wa Geita - Chato.

"Nawasihi wananchi wa Geita kujitokeza na kumpokea mgeni wetu, kwani hii ni fursa kwa mkoa wetu, tunapaswa kuitumia fursa hii vizuri" Amesema Mhandisi Luhumbi.