Rais wa China Xi Jinping amewaonya viongozi wa ulimwengu katika Jukwaa la Kiuchumi Duniani kwa njia ya video dhidi ya kuanzisha kile alichokiita Vita vipya Baridi na kuhimiza umoja wakati huu ambao dunia inapambana na janga la virusi vya corona. 

Akiuhutubia mkutano huo wa wiki moja ambao kawaida huandaliwa mjini Davos, Uswisi, Xi amesema kujenga makundi madogomadogo au kuanzisha Vita vipya Baridi ili kuwapinga, kuwatishia au kuwatishia wengine, kutausukuma ulimwengu katika mpasuko. 

Kiongozi huyo wa China pia ametoa wito wa kuwepo uongozi wenye nguvu duniani kupitia mashirika mbalimbali, kuondolewa kwa vizuizi vya biashara ya kimataifa, uwekezaji na mabadilishano ya teknolojia, pamoja na uwakilishi imara kwenye jukwaa la ulimwengu kwa nchi zinazoendelea.