Rais Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa Spika Job Ndugai kufuatia kifo cha mbunge wa viti maalum CCM, Martha Umbulla kilichotokea usiku wa kuamkia leo Alhamisi Januari 21, 2021 nchini India.

Taarifa iliyotolewa leo na mkurugenzi wa mawasiliano ya rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa kiongozi mkuu huyo wa nchi amepokea kwa masikitiko taarifa za mbunge huyo aliyekuwa Mumbai, India kwa ajili ya matibabu.

“Ametuma salamu za rambirambi kwa Ndugai, familia ya Martha, wabunge wote, wananchi wa Mkoa wa Manyara na wote walioguswa na kifo hicho.”

“Umbulla alikuwa mpole, mchapakazi na mpenda maendeleo. Nazikumbuka jitihada zake za uongozi akiwa mkuu wa Wilaya na akiwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Rais Magufuli.

Amewaomba wanafamilia wote wawe na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi kigumu cha majonzi na amemuombea Martha apumzike mahali pema peponi.