RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amelipongeza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kwa kuendelea na kazi kubwa ya kuimarisha amani na kuilinda mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Ulinzi Tanzania (CDF) Jenerali Venance Salvatory Mabeyo, aliyefika Ikulu Jijini Zanzibar kwa ajili ya kumpongeza.


Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limeendelea kufanya kazi kubwa ya kulinda amani nchini na kutoa pongezi maalum kwa kuisimamia amani hiyo hasa katika kipindi cha uchaguzi Mkuu uliopita.


Alisema kuwa wananchi wa Tanzania wanajivunia hatua hiyo ya Jeshi lao katika kuhakikisha wanakuwa salama wao pamoja na mali zao wakati wote na kumuhakikishia Jeneral Mabeyo kwamba Zanzibar iko salama.


Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba kutokana na kuwepo kwa ulinzi na usalama kumepelekea wananchi wa Zanzibar kuendelea kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo kwa amani.


Alisisitiza kwamba Zanzibar iko salama na kwa vile Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ)  lipo imara hatua hiyo imepelekea kuimarika zaidi.