Njombe:Watu wanne watiwa nguvuni kwa tuhuma za wizi wa nyaya za umeme
Na Amiri Kilagalila, Njombe
WAKATI Serikali ikielekeza nguvu kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na nishati ya umeme, mkoani Njombe watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi katika wilaya ya kipolisi mjini Makambako kwa tuhuma za kukutwa na nyaya za umeme zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 43 zinazotumika kusambazia umeme wa mradi wa REA.
Kamanda wa polisi mkoa wa Njombe Hamis Issa amesema hatua hiyo imekuja baada ya jeshi la polisi kufanya upelelezi wa kuwanasa watuhumiwa hao, kufuatia aliyekuwa msimamizi wa mradi wa Rea katika kata ya Kichiwa Tarafa ya Makambako kutoa taarifa kwenye jeshi hilo alipogundua dram sita za nyaya za umeme zenye thamani ya shilingi zaidi ya milioni 43 kuibwa .
“Tumekamata gari aina ya fuso na imebeba waya Rol zipatazo sita na hizi rol zipo nyaya za aina mbili tofauti zinazotumika kwenye umeme wa rea hapa mkoani Njombe”alisema Hamis Issa
Kamanda Issa amesema wamefanikiwa kukamata gari hilo kutokana na ufuatiliaji uliofanywa na vikosi vya polisi.
“Tuliweza kubaini kutokana na nyaraka iliyodondoka ya faini iliyotozwa hii gari,ikajulikana iko Dar Es Salaam,amefuatwa tajiri akasema gari iko Katavi na tulipofuatilia tuliikuta Mlele sehemu moja inatwa maji moto”alisema Kamanda Issa.
Vile vile ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuliamini jeshi hilo kwa kuwa lipo imara na watahakikisha jeshi linalinda miradi yote ya serikali hivyo wananchi wawe tayari kutoa taarifa miradi inapohujumiwa.