Kwa kawaida ndoa inapovunjika, uhusiano kati ya mwanamke na mashemeji hukatika pia. Lakini kwa Stella Mutahi, kuvunjika kwa uhusiano wake na mumewe kulizaa uhusiano mwingine usio wa kawaida.

Kaka yake mume wake aligeuka na kuwa mume wake wa pili.

Ilikuwaje hadi Stella akaolewa katika familia moja mara mbili?

tella anasema alikutana na mume wake wa kwanza wakati akisomea huduma za migahawa na mapishi na hata kabla ya kumaliza masomo alikuwa na ujauzito.

Baada ya kuhitimu kutoka chuoni Kikuyu, si mbali sana na jiji la Nairobi, hakurudi nyumbani kwao ila alichukua sanduku lake la nguo na kuanza maisha na baba wa mtoto wake.


Mwanamke huyu anasema kuwa maisha hayakuwa matamu katika ndoa ile ya kwanza kwa kuwa yule mpenzi wake alikuwa na hasira za mkizi. Stella alijihisi kana kwamba maisha yake yalikuwa hatarini .


Kifungua mimba wao akiwa na umri wa miezi minane, mambo yalizidi kuwa mabaya mno kwenye ndoa.


“Nakumbuka usiku wa mwisho wa ndoa yangu ya kwanza baba wa mtoto wangu wa kwanza alianza kunigombeza tukiwa chumbani. Mara ghafla akachomoza upanga uliyokuwa unawekwa pembeni pale chumbani,” anasema.

Nilidhani kuwa alikuwa na nia ya kunimaliza ila alinyanyuka ghafla na kuelekea nje pale ambapo gari langu lilikuwa limeegeshwa. Alianza kulikatakata, huku akivunja vioo vyote kwa upanga ule.”

Ni hapo ambapo wasiwasi ulijaa moyoni mwake na akaamua kujinusuru akiwa bado ana uwezo wa kufanya hivyo.

“Palepale nilihisi maisha yangu yakiwa hatarini, na nilichoweza kutoroka nacho ni mtoto wangu. Nilipewa pa kulala na jirani hadi asubuhi,” Stella anakumbuka.


Kesho yake mwanamke huyo alichukua uamuzi wa kutoka kwenye ndoa yake na kuanza maisha upya akiwa na mwanawe wa kike.


Haikuchukua muda kwa Stella kukutana na mpenzi mwingine japo mwanadada huyu anasema kuwa yule mwanaume alikuwa anamfahamu kabla ya kuingia chuoni.


Kwa hivyo ilikuwa tu kwamba urafiki wao ulipanda ngazi na kuwa wa kimapenzi.


Baada ya mwaka mmoja, mwaka wa 1999, waliamua kuanza kuishi pamoja kama mke na mume.


Maisha ya ndoa hii kulingana na Stella yalikuwa na changamoto zake ila yeye kama mwanamke alijizatiti kuvumilia kuifanikisha.


Walifanikiwa mabinti watatu.


Stella anasema kuwa changamoto kubwa katika ndoa yake ilikuwa kichapo cha karibu kila siku alichokuwa akikipata bila sababu.


Anasema kuwa mara nyingi mume wake alikuwa anarudi nyumbani na fujo ambazo hazikuwa zinaeleweka.


“Sikuwa ninaelewa hisia za mume wangu kwa kuwa asubuhi tukiamka alikuwa yuko sawa na mcheshi ila ifikapo jioni alikuwa anaanza kunitumia arafa za matusi na vitisho katika simu yangu ya mkononi.


“Nikizisoma hivyo tu, nilikuwa najua ningepokea kichapo cha mwaka usiku,” Stella anasema.


Na kwa kweli, mumewe aliporudi nyumbani jioni alianza kumzaba makofi na mateke bila sababu yoyote ila tu kutoa madai ya jinsi wanawake ni wabaya na kwamba wanawake ndio chanzo cha maisha yake kuharibika, anaeleza Stella.


Hakusema ni wanawake wangapi na wa wapi, ila ni swali ambalo Stella alikuwa anajiuliza kila wakati.


Kutokana na udhalilishaji huo, Stella alianza kuathirika kiakili. Watoto wake pia walimuogopa baba yao kama simba.


Akibisha jioni afunguliwe mlango, wote walikuwa wanatawanyika kama panya waliomsikia paka akiingia.


Stella anasema kuwa ni hali hiyo, pamoja na kutowajibika kwa mwanamume huyo kwa mahitaji ya nyumbani, iliyomlazimu kuanza kupanga njia ya kuondoka kwenye ndoa hiyo.


Stella anasema mwaka wa kumi wa ndoa hiyo ndio uliokuwa mbaya zaidi. Ilikuwa kila siku ni vita na matusi.


“Nakumbuka nikitamani nigongwe na gari. Kwa hivyo nikiwa mjini nilikuwa natembea hata katikati mwa barabara ili tu gari linigonge, angalau hata mguuni ili nilazwe hospitalini nisirejee nyumbani,” anasema.


Alikuwa akiwahurumia watoto wake, kwani alifahamu kuwa mazingira yale ya uoga na wasiwasi hayakuwafaa.