Shirika la Nyumba la Taifa litaanza kuwabana wapangaji wake wanaodaiwa takriban Bilioni 27 ikiwa ni malimbikizo ya upangishaji nyumba zake kwa kuwatangaza na kunadi mali zao kufidia deni kufikia mwisho wa mwezi Januari 2021.
Shirika hilo la nyumba la NHC lina takriban wapangaji 17,000 katika mikoa mbalimbali nchini zikiwemo taasisi za umma na binafsi wanaodaiwa kodi nyumba kama malimbikizo ya kodi hiyo baada ya kushindwa kulipa kwa wakati.
Akizungumza wakati wa kikao cha Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na watendaji wa Sekta ya ardhi jijini Arusha tarehe 9 Januari 2021 Meneja Huduma za Jamii na Uhusiano wa NHC Muungano Saguya alisema, kwa jiji la Arusha pekee shirika lake linadai wapangaji zaidi ya milioni 370 na kusisitiza kuwa zoezi hilo ni la nchi nzima.
Alisema, njia pekee kwa wadaiwa wa kodi ya pango la nyumba wa Shirika hilo kuepuka kuchukuliwa hatua ikiwemo kuwatangaza katika vyombo vya habari ni kuhakikisha wanalipa malimbikizo na kodi wanazodaiwa kabla ya januari 31, 2021.
Kwa mujibu wa Saguya, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linategemea fedha za wapangaji wake na miradi mbalimbali inayofanya kujiendesha hivyo kutolipwa fedha za upangishaji ni kufifisha juhudi za Shirika katika kujiendesha kibiashara.
“Shirika letu la NHC linategemea fedha za upangishaji nyumba zake na miradi kujiendesha kibiashara hivyo kutolipa kodi kunalifanya Shirika kushindwa kujiendesha kwa ufanisi” alisema Saguya.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema zoezi linaloendelea la kuwafikisha wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya liende sambamba na kuwachukulia hatua wapangaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wanaodaiwa kodi ya nyumba.
Alisema, Shirika la Nyumba la Taifa linategemea kwa asilimia mia moja kujiendesha hivyo wapangaji wake kushindwa kulipa kodi kwa wakati kunalifanya kushindwa kufanya kazi kwa ufanisi.
“Msako wa kodi ya ardhi pango la ardhi uende sambamba pia na wale wadaiwa wa Shirika la Nyumba la Taifa maana Shirika hujitegemea kwa asilimia mia moja, tusipolipa tutalikwamisha kufanya kazi” alisema Dkt Mabula.
Shirika la Nyumba la Taifa ni moja ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na mbali na upangishaji wa nyumba zake hujishughulisha pia na kazi mbalimbali kama vile ukandarasi wa miradi na upangaji miji ambapo kwa sasa linaendesha miradi ya ujenzi wa Hospitali za Rufaa za Mtwara na Kwangwa Mara, Ofisi za wilaya za Hai Kilimanjaro na Wanging’ombe Njombe pamoja na ujenzi wa Ofisi na nyumba 17 za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).