Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, WFM, Mwanza
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ilemela kuhakikisha vifaa tiba, umeme na maji vinapatikana kwa haraka katika Hospitali mpya ya Wilaya hiyo iliyojengwa katika eneo la Kabusungu  ili huduma za afya zianze kutolewa kwa wananchi kwa ufanisi.

Amelitoa agizo hilo baada ya kukagua ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na mradi wa Stendi ya Mabasi na Maegesho ya Malori kinachojengwa eneo la Nyamhongolo inayotekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Jijini Mwanza kwa ufadhili wa Serikali Kuu.

Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis ametoa maagizo hayo baada ya Uongozi wa Wilaya ya Ilemela kumweleza kuwa majengo muhimu ya hospitali hiyo yamekamilika lakini hospitali haijaanza kutoa huduma kikamilifu kutokana na kutopelekwa vifaa tiba pamoja na ukosefu wa umeme na maji katika eneo la mradi.

 “Serikali imetoa fedha nyingi kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kwa ajili ya kufanikisha ujenzi wa Hospitali hiyo hivyo haiwezekani ikabaki bila maji na umeme kwa kuwa ni muhimu katika uendeshaji wa Hospitali, lakini nawapongeza kwa ujenzi madhubuti wa hospitali, majengo ni mazuri na imara”, alisema Mhe. Mwanaidi Ali Khamis

Aliwataka watumishi wa Hospitali hiyo ambayo imeanza kutoa baadhi ya huduma kuhakikisha wanafanya kazi kwa bidii, uzalendo na kutunza vifaa na miundombinu iliyopo ili lengo la Serikali la kujenga hospitali hiyo na kuwapa wananchi huduma bora za afya liweze kutekelezwa kikamilifu.

Mchumi wa Manispaa ya Ilemela Bw. Mophen Mwakajonga, alisema kuwa majengo saba ya hospitali hiyo yaliyokamilika ni pamoja na jengo la wazazi, jengo la wagonjwa wa nje, utawala, maabara, mionzi na stoo ya dawa.

Alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.8 ambapo shilingi bilioni 1.7 zilitolewa na Serikali Kuu na shilingi milioni 176 zinatokana na mapato ya ndani ambazo zimetumika kufidia eneo la mradi na  kiasi cha shilingi milioni 304 zimetumika katika ujenzi wa ukuta wenye urefu kilomita 1.41 kuzunguka hospitali hiyo.

Katika hatua nyingine, akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi na maegesho ya malori-Nyamhongolo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango amemuagiza Mkandarasi  wa mradi huo kampuni ya Stecol Corporation kutoka nchini China, kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili uanze kufanyakazi kwa lengo la kuongeza mapato ya Manispaa na kukuza ajira kwa wananchi.

Alisema kuwa baada ya kukagua mradi huo amebaini kuwa haujakamilika kwa asilimia 65 kama watalaam walivyomweleza kwa sababu hata mafundi waliopo ni wachache na kuonesha wasiwasi wake kama mradi huo utakamilika mwezi Mei mwaka 2021 (mwaka huu) kama ilivyopangwa kwa mujibu wa mkataba.

Awali akitoa maelezo ya ujenzi wa Mradi huo wa Kituo cha Mabasi na maegesho ya Malori, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilemela Bw. John Wanga, alisema kuwa mradi huo utakaogharimu shilingi bilioni 28 umekamilika kwa asilimia 65 ambapo ukikamilika utakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 120  na kuegesha malori 100 kwa wakati mmoja.

Alisema kuwa mradi huo ukikamilika utachangia kuongeza mapato ya halmashauri, utachochea uchumi wa wananchi kwa kuzalisha ajira, pamoja na kubadilisha sura na mwonekano wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Dkt. Severine Lalika alimshukuru Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwa  kutembelea miradi hiyo na kuahidi kutekeleza maagizo yake yote ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi kwa kuongeza mapato ya Serikali na kuboresha huduma za afya.

Serikali kupitia Wizara ya Fdha na Mipango imetoa zaidi ya shilingi bilioni 288 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya kimkakati kwenye halmashauri 29 nchini, yenye lengo la kuziwezesha halmashauri kujitegemea kimapato na kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu.

Mwisho