Na. Farida Ramadhani na Peter Haule, Simiyu
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, Bw. Aswege Kaminyoge, kufanya uchunguzi wa gharama zilizotumika kujenga jengo la utawala la miradi ya kimkakati ya Chaki na Vifungashio wilayani humo baada ya kutoridhishwa na gharama zilizotumika ikilinganishwa na jengo hilo lilivyo.

Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis, ametoa agizo hilo Mjini Maswa, baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya miradi hiyo inayofadhiliwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 8.

Alisema kuwa jingo hilo lililokamilika kwa asilimia 93 ni la kawaida sana na haliwezi kugharimu shilingi milioni 178 fedha ambazo amesema ni nyingi ikilinganishwa na thamaniya jengo hilo ambalo mpaka sasa limejengwa kwa gharama ya shilingi milioni 110 kwa kutumia mfumo wa force account.

 “Tathmini ifanyike haraka na ripoti yake nipatiwe, lakini pia mkae muangalie namna ya kupunguza gharama, jengo lile haliwezi kutumia kiasi chote cha fedha hizo, lengo la Serikali ni kuzisaidia Halmashauri kujitegemea lakini sio kwa namna hii”, alisisitiza Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.

Aidha alimuagiza Mkandarasi wa SUMA JKT anayesimamia ujenzi wa Kiwanda cha Chaki na vifungashio kuhakikisha ujenzi wa majengo ya mradi huo yanakamilika kwa wakati ifikapo tarehe 15 mwezi Januari, 2021 kama alivyoelekeza Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo ili kazi ya kufunga mitambo ya kiwanda hicho ifanyike na  kuanza uzalishaji.

 “Tena tarehe 15 naona mbali, mimi naagiza tarehe 14, yaani kuanzia leo ufanyekazi usiku na mchana ili mradi huu ukamilike kwa wakati na vifaa viletwe kwa ajili ya kuanza kufanya kazi ili kutoa ajira kwa vijana pamoja na kuboresha mapato ya Halmashauri ambalo ndilo lengo la Serikali kuziwezesha Halmashauri zijitegemee na kuacha utegemezi wa ruzuku kutoka Serikali Kuu”, alisema Mhe. Mwanaidi Ali Khamis.

Naye Mbunge wa jimbo la Maswa Mashariki, Mhe. Staslaus Nyongo aliiomba Wizara ya Fedha na Mipango kutoa fedha kwa ajili ya kulipia mitambo ya kuchakata chaki iliyoko nchini Uturuki ili ifungwe kiwandani hapo na kuanza uzalishaji ili kuiwezesha Halmashauri ya Wialaya Maswa kuongeza mapato na kuwapunguzia wananchi mzigo wa michango ya miradi ya maendeleo ikiwemo elimu.

Mkuu wa Wilaya ya Maswa Bw. Aswege Kaminyoge alimhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwamba atatekeleza maagizo hayo na kusimamia kwa karibu zaidi utekelezaji wa miradi hiyo ili ikamilike kwa wakati na kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi hiyo ya Kimkakati.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Dkt. Fredirick Sagamiko alisema kuwa mwanzoni miradi hiyo miwili ya kiwanda cha kutengeneza chaki na kiwanda cha kutengeneza vifungashio ilitengewa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.2 lakini baada ya kufanya uchambuzi wa miradi hiyo, gharama imeongezeka hadi kufikia zaidi ya shilingi bilioni 29.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Bw. Festo Kiswaga kuhakikisha anajenga mindombinu ya barabara za hospitali mpya ya wilaya hiyo ili kuwawezesha wananchi kufika kwa urahisi na hudumiwa.

Alisema miundombinu iliyopo ya barabara za kuelekea hospitalini hapo zinaweza kusababisha madhara kwa wananchi hususani wagonjwa wanaohudumiwa katika hospitali hiyo hasa kipindi hiki cha mvua wakiwemo akina mama wajawazito na watoto.

Akizungumza na baadhi ya wagonjwa hospitalini hapo, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango aliwataka wananchi kutumia kikamilifu huduma za hospitali hiyo iliyojengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 1.9 na kusisitiza kuwa huduma za watoto waliochini ya umri wa miaka mitano zinatolewa bure.

Akitoa taarifa ya ujenzi wa Hospitali hiyo iliyoko katika kijiji cha Dutwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Bw. James John alisema hospitali hiyo imekamilika na imeanza kutoa huduma za afya kwa wananchi wakiwemo wagonjwa wa nje, wanaolazwa, huduma ya mama, baba na mtoto, tiba na matunzo ya wagonjwa wa kifua kikuu na ukoma.

Aliiomba Serikali isaidie upatikanaji wa watumishi wa kada mbalimbali, vifaa tiba ikiwemo vifaa vya upasuaji, vitanda vya kujifungulia, mashine za kutolea dawa ya usingizi, ultrasound, samani pamoja na gari la kubebea wagonjwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Bw. Festo Kiswaga, alimweleza Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis kwamba miundombinu ya barabara itawekwa kuunganisha majengo ya hospitali ili kuondoa adha ya wagonjwa kutembea kwenye tope hasa wakati wa mvua.

Mwisho.