Na Allawi Kaboyo -Biharamulo.
Naibu waziri wa Nishati Mhe. Adv. Stephen Byabato na Mbunge wa Jimbo la Bukoba amefanya ziara ya kikazi wilayani Biharamulo na kutembelea kituo Cha kupozea umeme kinachojengwa Nyakanazi wilayani humo ikiwa ni ufatiliaji wa maelekezo ya waziri wa wizara hiyo aliyoyatoa wakati wa ziara yake mwezi Desemba mwaka Jana.

Akiwa katika ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo amepokea taarifa ya hali ya umeme kutoka kwa mkuu wa wilaya kanali Mathias Kahabi ambaye ameeleza kuwepo kwa changamoto ya kukatika kwa umeme wilayani humo ambayo imekuwa kero sugu.

Mkuu huyo wa wilaya ameeleza kutoridhishwa na Kasi ya usambazaji wa umeme kwa vijiji 25 ambavyo waziri wa Nishati Mhe. Medard Kalemani aliagiza vipelekewe umeme ambapo amesema maagizo hayo hayajatekelezwa huku akiongeza kuwa wananchi wamekuwa wakipewa bei mkanganyiko za uunganishwaji wa umeme tofauti na maelekezo ya serikali.

Akitolea ufafanuzi wa changamoto hizo Naibu waziri Byabato amemtaka Meneja wa TANESCO wilaya Biharamulo Erenest Milyango kuandika barua kwa mkurugenzi mtendaji wa shirika hilo nchini Dkt. Tito Mwinuka  kueleza sababu zinazopelekea kukatika hovyo kwa umeme wilayani humo.

"Ninachojua umeme hapa nchini tunao wa kutosha hivyo hatutarajii kuwa na sababu zisizo za msingi zinazopelekea kukatika kwa umeme hasa kwa wilaya hii ambayo tayari ipo kwenye grid ya Taifa, Bahati nzuri nimekuja na mkurugenzi mtendaji wa TANESCO naelekeza kufika mwishoni mwa wiki ijayo nipate barua ya kuonyesha sababu za kitaalamu kuhusu suala hili" amesema Byabato.

Byabato amewaelekeza wataalamu wote wa TANESCO NA REA nchini kuwa Bei ya uunganishaji wa umeme kwa wananchi walioko vijijini ni shilingi elfu 27,000/= tu na si vinginevyo na kuongeza kuwa umeme unatakiwa kuwafuata wananchi kwenye maeneo yao.

Akiwa katika ujenzi wa kituo cha kupozea umeme Nyakanazi kinachojengwa na  kampuni ya LARSEN & TURBO COP. LTD ya nchini India kwa gharama ya zaidi shilingi bilioni 22, amepongeza hatua ambayo ujenzi umefikia na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa muda uliopangwa.

Aidha Naibu waziri amesema kuwa kituo hicho ni kitovu cha umeme kwa Mkoa wa Kagera hivyo ukamilishwaji wake unatakiwa kwenda sambamba  na ujenzi wa njia za kusafirishia umeme kwenda kwa wananchi ambapo itawezesha mkoa mzima kuanza kutumia umeme wa Grid ya Taifa na kuachana na umeme tegemezi.

"Nimekuja hapa kufatilia maagizo ya Mhe. waziri Medard Kalemani aliyoyatoa mwishoni mwa mwaka Jana kuhusu kituo hiki Kama yametekelezwa, lakini pia Kama mnakumbuka Mhe. Rais Magufuli alinipa kazi Maalumu ya kuhakikisha mkoa huu unaingia kwenye Grid ya Taifa, Sasa nataka kujua maelekezo hayo yametekelezwa kwa kiasi gani?." amesema  Byabato.

ameongeza kuwa mradi huo unatakiwa kukamilika tarehe 31 Mach, mwaka huu na kuanza kusambaza umeme kwa wananchi na kumtaka mkandarasi kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa.

Awali akitoa taarifa ya Maendeleo ya mradi huo meneja  wa mradi Sospiter Olaro ameeleza kuwa ujenzi wa Mradi umefikia asilimia 60% huku changamoto kubwa ikiwa ni kuchekeweshwa kwa transformer zilizokwama bandarini kwa kushindwa kulipiwa gharama za usafiri kuwa juu.

Akitolea ufafanuzi wa changamoto hiyo, Mhe. Byabato amesema kuwa suala Hilo atakwenda kulishughulikia kwenye wizara husika ili kuhakikisha kazi hiyo haisimami.