Na Munir Shemweta, WANMM KILIMANJARO
Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula ameshangazwa na halmashauri za mkoa wa Kilimanjaro kuingia mikataba ya urasimishaji na makampuni zaidi ya nane ambayo yameshindwa kukamilisha kazi suala lililosababisha makampuni hayo kuanza kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU). 


Akizungumza na Uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro, Wakurugenzi wa Halmashauri, watendaji wa sekta ya ardhi na Makampuni ya urasimishaji katika kikao chake kilichofanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkoa wa Kilimanjaro tarehe 8 Januari 2021 akiwa katika ziara ya siku moja, Dkt Mabula alisema haiwezekani wakurugenzi wote wa halmashauri kuingia mikataba na makampuni zaidi ya nane ya urasimishaji katika mkoa na yashindwe kukamilisha kazi.


” Wakurugenzi wote mko hapa wakati mnaingia mikataba na makampuni ya urasimishaji mliwachunguza kabla ya kuingia mikataba? maana haiwezekani mkoa mzima makampuni yashindwe kukamilisha kazi kwa wakati na naagiza halmashauri zifanye uchunguzi kabla ya kuyapa kazi makampuni” alisema Dkt Mabula.


Alisema, Makampuni ya upimaji hayatakiwi kwenda kinyume na mpango uliowekwa na halmashauri na yanatakiwa kufanya kazi kwa kwenda mtaa kwa mtaa na siyo mtu kwa mtu na kuongeza kuwa halmashauri zinatakiwa kuyachunguza na kuchukua makampuni yenye uwezo na mtaji na siyo kutegemea fedha za wananchi. 


Aliiagiza Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji na Makampuni kuyachunguza makampuni yote ya urasimishaji ambayo hajakamilisha kazi na wakibaini kampuni zisizo kuwa na uwezo basi zifutwe kufanya kazi tena ya upangaji na upimaji nchini.


Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi aliongeza kwa kusema kuwa, Wizara ya Ardhi iliona jambo jema kushirikisha sekta binafsi katika zoezi la urasimishaji kwa lengo la kuongeza kasi ya upimaji  na kusisitiza kuwa Wizara ya Ardhi inachotaka ni Kampuni inayopewa kazi ni kuwa na angalau asilimia 50 ya mtaji wa kufanya kazi badala ya kutegemea fedha za wananchi.


“Wizara inasema kama huna fedha usitegemee pesa  za wananchi kuendesha kazi ya urasimishaji na tusiwafanye wananchi ndiyo mtaji kwa kuwa mwisho itakuwa kero kwa kushindwa kukamilisha kazi” alisema Dkt Mabula.


Mkurugenzi Mtendaji wa moja ya Kampuni za Urasimishaji katika mkoa wa Kilimanjaro ya KILI Surveys LTD Alphonce Mwanshinga alijitetea mbele ya Naibu Waziri Dkt Mabula kwa kueleza kuwa kampuni yake tayari imeshapima viwanja 2,795 na kulipwa shilingi milioni 283,361 huku ikiendelea kudai milioni 247,639,000 kutoka kwa wananchi.


Hata hivyo, alisema changamoto kubwa kwa kampuni yake kushindwa kukamilisha zoezi hilo kwa wakati ni kuwa walipoanza kazi waliendesha zoezi kulingana na uitikio wa wananchi na kuamua kupima kwa wale waliolipa fedha na kuongeza kuwa kampuni yake ya KILI Surveyers LTD inatarajia kukamilisha zoezi la upimaji katika mtaa waliopewa mwisho wa mwezi Januari 2021.


Baadhi ya Makampuni yaliyopewa kazi ya urasimishaji kwenye mkoa wa Kilimanjaro ni pamoja na Kili Surveys Ltd, Makazi Solution, EM& Contruction Ltd, Land Surveys and Consultancy Services pamoja na Kampuni ya EM Land Consultants.