Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amebaini ubadhilifu wa zaidi ya Bilioni 2 uliofanywa na Wakufunzi wa Chuo Cha Ardhi Morogoro (ARIMO) na kumuelekeza Mkuu wa Chuo Huruma Lugala kumsimamisha  kazi mara moja Mkuu wa Utawala wa Chuo Michael Lori kwa  tuhuma ya kushirikiana na wakufunzi wawili wa chuo hicho waliofanya ubadhilifu katika zoezi la urasimishaji.

Dkt Mabula alitoa maelekezo hayo mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro wakati akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na uongozi wa mkoa wa Morogoro akiwa katika ziara yake ya siku moja kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na miradi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Alisema, Wizara yake ilifikiri kushirikisha makampuni binafsi katika zoezi la urasimishaji ingerahisisha kazi ya kupima na kumilikisha wananchi maeneo yao lakini matokeo yake baadhi ya makampuni na watu wachache wametumia nafasi hiyo kufanya ulaghai wa kuchukua fedha za wananchi bila kukamilisha kazi ya urasimishaji.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mkuu wa Utawala katika Chuo cha Ardhi Morogoro ameonekana kushirikiana na watuhumiwa kwa namna moja ama nyingine na uamuzi wa kumsimamisha ni kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.

Naye, Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Mhandisi Emanuel Kalobelo ameeleza namna anavyosikitishwa na baadhi ya watumishi wa sekta ya ardhi mkoani hapo wanavyofanya Kazi na kumtia aibu katakana na utendaji wao mbovu, na ameahidi kuwasimamia kikamilifu ili muleta ufanisi.

Awali Dkt Mabula alielezwa na Mkuu wa Chuo cha Ardhi Morogoro Huruma Lugala kuwa wakati uongozi wa chuo hicho ukifanya jitihada za kukiboresha chuo ikiwemo kudhibiti hujuma mbalimbali ilibainia baadhi ya Wakufunzi wake kujihusisha na kazi ya urasimishaji katika maeneo mbalimbali kwa kutumia jina la chuo kujipatia fedha.

Alisema, chuo chake baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na kubainia udanganyifu kwa baadhi ya watumishi wake kiliamua kuwasimamisha Wakufunzi wawili kupisha uchunguzi na kuwataja watumishi hao kuwa ni Adolf Milungala anayetuhumiwa kujipatia shilingi Bilioni 1.9 na Hamis Abdalah Kindemile milioni 275 fedha zilizokuwa malipo ya urasimishaji katika mitaa 43 Morogoro.