Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma
Wafamasia wote nchini wametakiwa kutoishia kutoa dawa kwa wagonjwa bali kusimamia ili kujua kama dawa zimefika kwa mgonjwa.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel wakati wa mahafali ya kiapo cha wafamasia wanaoingia katika taaluma iliyofanyika jijini hapa.

Akiongea wakati wa sherehe hizo Dkt. Mollel amesema kuwa wafamasia hao wanalo jukumu kubwa la kuokoa maisha ya wananchi hivyo kutokuhakikisha dawa walizotoa zinamfikia mgonjwa ni kupoteza maisha kwa wagonjwa wanaofika kupata huduma kwenye vituo vyao.

“Wizara inawategemea sana na kutambua kazi kubwa inayofanywa na wafamasia licha ya wachache waliopo kuiangusha taaluma hiyo,hii ni kuvunja kiapo mlichoapa leo na kituo kinapokosa dawa wapo wananchi wanaopoteza maisha na unapokuta upotevu wa dawa lazima mfamasia ahusike”.
Alisema Dkt. Mollel.

Hata hivyo Naibu Waziri huyo amewata wafamasia hao walioingia rasmi leo kwenye taaluma wasisubiri kuingiza dawa au kumpatia mgonjwa dawa bali wametakiwa kuwa wabunifu kwa kutengeneza dawa kwenye maeneo yao kazi ili kuweza kuipunguzia gharama Serikali.

“Mtakapoenda kwenye ajira nataka mjue eneo la dawa ni muhimu sana kwenye uhai wa hospitali hivyo mkiisimamia vyema serikali itakaa vizuri, muhakikishe mnasimamia vizuri eneo hilo hususani kwenye maamuzi katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini”.

Kwa upande wa matumizi ya fedha Dkt. Mollel amewataka wafamasia kuwajibika ipasavyo kwani kumekuwepo na matumizi mabaya ya fedha za dawa kwenye vituo vya umma na hivyo kusababisha kukosekana kwa dawa na vitendanishi na hivyo kusababisha wananchi kutojiunga na bima za afya ikiwemo CHF na wengine wenye uwezo kukimbilia kwenda kwenye hospitali binafsi.

Naye Msajili wa Baraza la Famasi Bi. Elizabeth Shekalaghe amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye dawa hivyo wanapaswa kusimamia kikamilifu huduma zote za famasi kwa kuzingatia sheria,kanuni, taratibu ,vigezo vilivyopo ,maadili na miiko ya utendaji kazi za kila siku.

“Tumesisitiza sana suala ya uwajibikaji,tunafahamu taalama ya famasi imeanza toka mwaka 1978, lakini ukuaji wake umekua kwa taratibu sana ila hivi sasa imekua ikiongezeka kila mwaka na wastani kila mwaka wanahitimu wanafunzi wasiopungua 250 na hivyo tumeweza kusajili wafamasia 2329 hadi sasa”.Alisema.

Shekalaghe amesema Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye sekta ya afya ikijumuisha huduma zitolewazo ikiwemo huduma za dawa“Mhe Rais ametuona hivyo hatupaswi kumuangusha tuhakikishe tunasimamia kikamilifu rasiliamali hizi ambazo serikali imewekeza katika utoaji wa huduma za dawa”. Alisisitiza Shekalaghe.

Hata hivyo amesema, katika mahafali hayo wameweza kujadili namna gani wanaweza kutumia mifumo iliyopo ili kuweza kufanya huduma zinazotolewa katika mnyororo wa dawa, kusimamiwa na kuhakikisha dawa zinawafikia wagonjwa kwa kuweka kumbukumbu vizuri.

Wakati huo huo mwakilishi wa wahitimu hao Mkapa Madebele amewaasa wahitimu wenzie kufuata na kuzingatia sheria za taaluma yao kwani wanahusika kila siku kwenye famasi na kutaka kulinda weledi kwani afya za wananchi zipo juu yao.

Madebele amesema wapo tayari kutumika na kuajiriwa sehemu yoyote nchini ili kuwasaidia wananchi ambao ndio wazazi na walezi wao kwenye jamii kama wanataaluma wa dawa.

Baraza la Famasi moja la jukumu lao ni kuwasajili wanataaluma hao waliokidhi vigezo, jumla ya wahitimu 252 wamehitmu katika mahafali ya tisa yanayofanyika kila mwaka kwa awamu mbili.