Mwanaume aliyejulikana kwa jina la David Makerege Mluli (80) amekutwa amefariki dunia ndani ya Hoteli ya Mbezi Garden iliyopo Mbezi jijini Dar es salaam akiwa na mpenzi wake aliyejitambulisha kwa jina la Neema Kibaya (33). Kifo hicho kilitokea muda mfupi tangu wafike hotelini hapo, kwa mujibu wa maelezo ya polisi.
Taarifa ya kifo hicho ilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii juzi na jana, huku ikielezea namna tukio lilivyokuwa kwa wawili hao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyokuwa ikizunguka mtandaoni, marehemu ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika katika hoteli hiyo huku akiwa na maji na juisi katika chumba alicholipia.
Neema alipofika inasaidikika kuwa aliagiza chipsi na mishikaki mitatu. Walipokuwa pamoja Neema aliona ghafla mzee huyo akipumua kwa shida ndipo alipokwenda kutoa taarifa mapokezi akiomba msaada.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Ramadhan Singai alisema tukio hilo lilitokea Januari 16, 2021 katika hoteli hiyo huku akibainisha kuwa uongozi wa hoteli ndiyo uliopiga simu kuripoti jambo hilo.
“Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa meneja wa hoteli hiyo aitwaye Newton Mkonda kuwa katika chumba namba 22 kuwa kuna mteja amefariki dunia.
“Baada ya taarifa kupokelewa jeshi la polisi lilifika katika eneo la hoteli hiyo na kubaini uwepo wa maiti ya mwanaume ambaye jina lake lilifahamika kupitia kitambulisho kilichokuwapo katika nguo zake,” alieleza Kingai.
Alisema mbali na maiti pia katika chumba hicho alikutwa Neema ambaye alijitambulisha kama mpenzi wake marehemu na mkazi wa Goba jijini hapa.
“Katika uchunguzi wa awali uliofanyika, jeshi la polisi lilibaini kuwa mwili wa marehemu haukuwa na jeraha lolote. Mwili ulichukuliwa na askari waliofika na kupelekwa katika hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya kuhifadhiwa,” alisema kamanda huyo.
Alisema katika uchunguzi huo pia walibaini kuwa kifo cha marehemu ni cha kawaida kwani licha ya kutokuwa na jeraha ni mkojo pekee ndiyo walibaini ulikuwa umemtoka.
“Bado hatujafikia hitimisho kwani bado tunahitaji kufanya uchunguzi zaidi hasa kupitia kwa madaktari ili kujua kuwa kifo hiki kimetokea kwa sababu gani.
“Tunasubiri ndugu wa marehemu, katika taratibu za uchunguzi lazima kuwe na mtu anatambua mwili huo, sisi tumetambua kwa kupitia vitambulisho na kuoanisha sura yake na iliyopo kwenye vitambulisho, lakini katika uchunguzi wa hospitali hasa ndugu ndiyo wanaopaswa kuthibitisha kuwa huyu ndiyo yule ambaye sisi tunasema amefariki,” alieleza.
Kuhusu Neema alisema anashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.