Dar es Salaam. Justina Gerald (15) mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Canossa aliyeshika nafasi ya kwanza kwa wasichana katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2020 amesema anataka kuwa mhandisi wa mafuta.


Mbali na kuwa wa kwanza kwa wasichana katika mtihani huo, Justine aliyesema siri ya kufaulu ni kumtanguliza Mungu katika masomo,  ameshika nafasi ya pili katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa.


 “Kwanza ni kumtanguliza Mungu kwa kila jambo, pia ni kuweka nia na malengo na kuhakikisha nayatekeleza na pia kushirikiana na wanafunzi wenzangu na walimu na wazazi,” amesema Justina alipozungumza na Mwananchi Digital.


Kuhusu matarajio yake amesema anataka kuwa mhandisi wa mafuta na ndio kozi  anayotamani kuisoma atakapojiunga chuo kikuu.


 “Nataka kuwa mhandisi wa mafuta ya petroli kwa sababu nchi zinazoendelea kama Tanzania ndiyo zinategemea kukuza uchumi wake,” amesema Justina.