TAARIFA ya moto ikufikie kwamba, ule msamaha wa msanii wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ kwenda kwa baba yake aliyemlea kimuziki, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, umeibua mazito, RISASI MCHANGANYIKO lina ‘exclusive’.

Habari za ndani kabisa kutoka kwenye lebo inayosimamiwa na Diamond au Mondi ya Wasafi Classic Baby (WCB), zinaeleza kuwa, jamaa huyo amekataa kweupe kuukubali msamaha huo.

 

UNAFIKI MTUPU?

Vyanzo hivyo vinadai kwamba, miongoni mwa sababu alizozitoa Mondi ni kwamba ukisoma maelezo ya Harmonize au Harmo utagundua yana unafiki mtupu ndani yake.

 

“Mbali na unafiki, pia kuna kitu kingine Simba (Mondi) amekinotisi kwenye maelezo ya Harmonize.

“Simba anasema Harmonize anamshukuru kwa kumkuza kimuziki kiasi kwamba kwa sasa anajiona ni mkubwa kuliko hata yeye (Mondi) mwenyewe.

“Unajua huyu dogo (Harmo) kwa sasa anajiona amevimba kichwa na kujiona yupo juu kuliko hata Simba (Mondi) mwenyewe.

 

MBAVU HAELEWEKI?

“Kiukweli anachokisema Simba (Mondi) ni kwamba Mbavu (Harmo) haeleweki kuanzia yeye mwenyewe hadi timu yake nzima.

“Simba (Mondi) anasema haelewi huyo jamaa (Harmo) anatengeneza nini hasa.

“Kuna muda huwa anamuona bora angeendelea kubaki Wasafi tu atengeneze lebo yake ndani ya Wasafi kama wanavyofanya akina Rayvanny sasa hivi.

 

ANGEKUWA KAMA EMINEM?

“Huwa Simba (Mondi) anatoa mifano mingi tu ya wasanii wakubwa duniani wa mbele kama Eminem, bado yupo chini ya Lebo ya Dr Dre ya Aftermath Entertainment, lakini naye ana lebo yake ya Shady Records ambayo inamsimamia yeye pamoja na wasanii wengine aliowasaini.

 

“Huyo Mbavu (Harmo) alipotoka Wasafi ilitakiwa aweke nguvu zaidi kwenye kazi zake, abamize kazi tu.

“Sasa tatizo linakuja pale anapochanganya Uswahili na kazi, anasahau kwamba Simba ambaye ni bosi wake wa zamani amekulia eneo ambalo lina kiini cha Uswahili wenyewe.

 

AKUMBUSHWA YA BOB JUNIOR

“Simba (Mondi) anasema anamkumbusha enzi za Bob Junior ambaye alipotaka kushindana naye alianguka vibaya, lakini wakati wa bifu lao, wala Simba hakuwa anakazana kubishanabishana na Bob Junior.

“Yeye (Mondi) anasema alichokifanya ni kukazania muziki wake tu na sasa wengi wanajua kilichompata Bob Junior na sasa anafanya nini mjini wakati kipindi hicho alikua na moto mkubwa.

 

“Simba anasema kuwa, hakuna ambaye hajui kwamba yeye ndiye aliyemtoa Mbavu (Harmo), lakini kitendo cha kutaka kuwa hasimu wake hakikumfurahisha kuona kinyago alichokichonga mwenyewe sasa kinamtisha.

 

ANATAFUTA HURUMA?

“Simba anasema kama Mbavu aliona kuna mahali hakutendewa haki, basi angekuwa wazi kuliko kutumia jina la Simba kutafuta huruma kwa watu na kuna muda inabidi ajiangalie ni nini hasa anataka.

“Simba anachosema ni kwamba, sawa, Mbavu aliamua kujitoa Wasafi, lakini kilicholeta shida ni jamaa kuleta maneno badala ya kujenga ngome yake ya kimuziki iwe imara kwanza,” kilihitimisha chanzo hicho.

 

BABU TALE ANASEMAJE?

Akizungumza na gazeti hili kuhusu hicho kinachotajwa kama msamaha wa Harmo kwa Mondi, mmoja wa mameneja wa Wasafi, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ anasema kuwa, hilo ni jambo la kawaida tu na wao hawana lolote la kujibu.

“Hakuna lolote, ni kawaida tu…”

 

MENEJA WA HARMO SASA

Kwa upande wake, mmoja wa mameneja wa Harmo, Rajab Mchopa anasema kuwa kwa upande wao kama uongozi hawana lolote la kusema, badala yake Harmo ndiye mwenye jukumu la kuzungumzia ishu hiyo.

 

MONDI NA HARMO

Harmo alijitoa kwenye Lebo ya Wasafi mwaka juzi na kwenda kuanzisha lebo yake maarufu kwa jina la Konde Gang Music Worldwide.

Baada ya kujitoa, uongozi wa Wasafi ulimwekea ngumu kutumia nyimbo alizozalisha akiwa chini ya lebo hiyo hadi pale alipolipa shilingi milioni 500 kama ada ya kuvunja mkataba na kuanzia hapo akawa huru.

Lakini kitendo hicho kimeendelea kuchukuliwa tofauti na mashabiki wao na kusababisha kuwepo kwa bifu baina yao ambalo hadi leo limeendelea kufukuta.