Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, – Aboubakar Kunenge, jana amekagua madarasa katika shule ya msingi King’ongo iliyopo wilayani Ubungo.

Kunenge amekagua madarasa hayo kufuatia agizo lililotolewa mapema jana  mkoani Kagera na Rais Dkt John Magufuli la kuwataka Viongozi wa wilaya ya Ubungo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kuhakikisha atakaporejea jijini Dar es salaam, madarasa katika shule hiyo yawe yamekamilika na Wanafunzi hawakai chini.

“Ninazungumza nikiwa Kagera, lakini nikienda Dar es salaam niyakute hayo madarasa yamekamilika na Wanafunzi hawakai chini,” aliagiza Rais Magufuli.

Akitoa agizo hilo Dkt Magufuli amesisitiza kuwa haiwezekani kuwa amewapa watu madaraka, wanazunguka kwenye maeneo hayo lakini bado wanafunzi wanakaa chini.