IMEELEZWA kuwa, kiungo wa Simba, Jonas Mkude anatarajia kupigwa faini na uongozi wa timu hiyo kutokana na kosa la kinidhamu alilolifanya ili aweze kurudi kikosini.

 

Mkude alisimamishwa kwa muda usiojulikana tangu mwanzoni mwishoni mwa mwaka jana kutokana na kosa la utovu wa nidhamu alioufanya wa kuchelewa mazoezini na masuala mengine ambayo uongozi wa klabu hiyo haukuwekwa wazi.

 

Hadi sasa Mkude tayari ameshakosa mechi kadhaa za ligi kuu, mechi ya kimataifa dhidi ya FC Platinum iliyowavusha Simba hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Taarifa ambayo Championi Jumatano, imezipata kutoka ndani ya Simba inasema kuwa, uongozi unatarajia kumpiga faini kiungo huyo mara baada ya kikao cha kamati ya nidhamu kukaliwa hivi karibuni ili aweze kurudi kundini.“

 

Mkude bado ni mchezaji wa Simba na hivi karibuni atarejea kundini awali kamati ilikuwa inasubiria michuano ya Kombe la Mapinduzi iweze kufikia tamati ndipo ipange siku ya kukutana ambayo watakutana ili kujadili juu ya suala la Mkude ambapo atapigwa faini ili aweze kujiunga na wenzake wakati wowote kuanzia sasa kwani ni mmoja wa wachezaji wanaotegemewa,” alisema mtoa taarifa huyo.

 

Mkataba wa Mkude na Simba unatarajia kufikia tamati Juni mwaka huu.

Stori na Khadija mngwai, Dar es Salaam