Sherehe za uzinduzi wa michuano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani yaani CHAN kwa msimu huu wa mwaka 2021 zinataraji kufanyika usiku wa leo wa tarehe 16 januari 2021  nchini Cameroon ambapo michuano hiyo inataraji kuanza kwa michezo miwili ya ufunguzi.

 Sherehe za uzinduzi wa michuano hiyo ambayo inafanyika kwa msimu wa sita tokea kuanzishwa kwake mwaka 2009, zitaambatana na tukio maalum ya kumkabidhi tuzo ya heshima ya uongozi uliotukuka kwa Issa Hayatou aliyekuwa rais wa CAF kuanzia mwaka 1988 hadi 2017.


Hayatou anatazamiwa kukabidhiwa tuzo hiyo ndani ya ardhi ya nchini kwake Cameroon na muwakilishi wa shirikisho la soka la barani Afrika anayekaimu nafasi ya Ahmad Ahmad aliyefungiwa kujihusisha na soka kwa muda wa miaka mitano kufuatia tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.


Sherehe ya ufunguzi wa michuano hiyo itazinduliwa na mgeni rasmi wake rais wa shirikisho la soka Duniani FIFA, Gianni Infatino ambaye ataambata na viongozi wa mashirikisho mbalimbali Afrika na mwenyeji wake Seydou Mbombouo anayekaimu nafasi ya urais wa shirikisho la soka nchini Cameroon


Michuano hiyo inashirikisha timu za taifa kutoka mataifa 16 ambazo zipo kwenye mfumo wa makundi 4 kila kundi likiwa na timu 4 ambapo vinara na washindi wa pili wa kila kundi watafuzu kucheza hatua za mtoano kuanzia robo fainali mpaka fainali kwa wale watakaokuwa wanashinda.


Michezo miwili ya ufunguzi ni ile kutoka kundi A, wenyeji Cameroon kufungua pazia  na Zimbabwe saa 1:00 usiku ilhali timu ya taifa ya Mali itakipiga na timu ya taifa ya Burkina Faso mchezo mishale ya saa 4:00 usiku yote kwenye dimba la  Amadou Ahidjo jijini Yaounde.


Michezo miwili mingine itaendelea tena usiku wa kesho jumapili ya tarehe 17 Januari 2021 kwa michezo miwili, kutoka kundi B, Libya itakipiga na Niger saa 1:00 usiku, DR Congo dhidi ya Congo saa 4:00 usiku, kundi C Morocco bingwa mtetezi atapepetuana na Togo saa 1:00 usiku wa Jumatatu.


Rwanda na Uganda ni mchezo mwingine kutoka kundi C utakaochezwa siku ya Jumatatu tarehe 18 Januari 2021 mishale ya saa 4:00 usiku ilhali michezo ya kundi D itachezwa siku ya Jumanne tarehe 19 Januari 2021 ambapo Zambia itaumana na Tanzania saa 1:00 usiku na Guinea na Namibia 4:00 usiku.


Mshindi wa kwanza wa michuano hiyo anatazamiwa kuondoka na kitita cha dola za kimarekani milioni  1,250,000 ambazo ni sawa na zaidi ya bilioni 2, milioni 890 za kitanzania, mshindi wa pili atapata dola 700,000 za kimarekani ambazo ni sawa na zaidi ya bilioni 1, milioni 600 za kitanzania.


Mshindi wa nne atapata dola za kimarekani 400,000 ambazo ni sawa na zaidi ya milioni 926 na laki 400 ilhali mshindi wa nne atapata dola 300,000 za kitanzania ambazo ni sawa na milioni 694 na laki 800 a kitanzania. Zawadi hizo zitatolewa mwisho wa mashindano hayo tarehe 7 februari 2021.