BONIFACE Amani Gichina, Mchungaji wa Kanisa la Living Faith Church maarufu Winners’ Chapel International, nchini Kenya amefungwa jela miaka 140 kwa kuwapa mimba mabinti zake wawili. Inaripoti BBC … (endelea).

Anthony Mwicigi, Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Baricho nchini humo, amemuhukumu Mchungaji Gichina (51) kwa ubakaji wa watoto wake wenye miaka 14 na 16.


Tayari mabinti zake hao wamejifungua, mmoja akiwa na mtoto wa miezi saba na mwingine miezi mitano.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Anthony amemuhukumu mchungaji huyo kifungo cha miaka 70 kwa kila binti yake, na kueleza hukumu hizo zitatekelezwa moja baada ya nyingine.

Mhungaji Gichina anayetoka katika Kaunti ya Kirinyaga, mbele ya mahakama hiyo, alikiri kubaka watoto wake na kisha kuwajaza mimba.


Mchungaji huyo baada ya kufanya hivyo na kubaini anatafutwa, alitoweka lakini alikamatwa kutokana na msako ulioondeshwa na polisi.

Ameiambia mahakama hiyo, amerubuniwa na shetani na kusababisha kuwaingilia mabinti zake wote na hivyo, anamlaumu kwa kumrubuni na kutenda kosa hilo.


Kutokana na kosa hilo, amewaomba msamaha watoto wake pamoja na mahakama.