UPO uwezekano mkubwa wa mshambuliaji wa kimataifa wa Yanga Mghana Michael Sarpong kuondoka kati ya mwanzoni au mwisho mwa msimu huu baada ya kupata dili la kucheza nje ya nchi.


Mghana huyo hivi sasa ameonekana kutokuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Mrundi Cedric Kaze mwenye mabao manne pekee katika msimu huu wa Ligi Kuu Bara.


Awali, Yanga ilikuwa ina matarajio makubwa na Mghana huyo kabla ya kujiunga na timu hiyo katika msimu huu akitokea Rayon Sports ya nchini Rwanda.


Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, mshambuliaji huyo yeye mwenyewe ndiye anataka kuondoka baada ya kupata ofa kwenye moja ya klabu ya nje ya nchi.


Mtoa taarifa huyo alisema kuwa mshambuliaji huyo tayari ameutaarifu uongozi wa timu hiyo, lakini bado hajapatiwa majibu juu ya suala hilo.Aliongeza kuwa kama uongozi utakubaliana na mshambuliaji huyo, basi upo uwezekano mkubwa wa kuondoka katikati ya msimu au mwishoni baada ya ligi kumalizika.


“Sarpong hivi karibuni aliutaarifu uongozi juu ya yeye kupata ofa nzuri ya kwenda kucheza soka nje ya nchi baada ya kupata ofa nzuri.


“Lakini uongozi bado haujampa majibu juu ya hilo, bado mazungumzo yanaendelea kama yakienda vizuri, basi ataondoka Yanga na kwenda huko anapotaka kwenda,” alisema mtoa taarifa huyo.


Alipotafutwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga Injinia, Hersi Said kuzungumzia hilo simu yake ya mkononi iliiita bila ya mafanikio ya kupokelewa.

STORI: WILBERT MOLANDI, Dares Salaam