MAMA mzazi wa msanii maarufu wa Bongo Fleva, Diamond Platinumz, Bi. Sandrah,  ameamua kumaliza utata na kuweka wazi kuwa Mzee Abdul Juma ambaye wengi wanamjua kama baba mzazi wa Diamond, si baba Mzazi wa Diamond kwani wakati wanaingia kwenye mahusiano, tayari mama huyo alikuwa na ujauzito wa mwanamuziki huyo.

 

Bi. Sandrah amefunguka hayo leo kupitia kipindi cha MashamSham, kinachoruka kupitia Wasafi FM baada ya kupigiwa simu LIVE kufuatia mahojiano ya Ricardo Momo ambaye ameelezea kuwa ni kaka yake na Diamond kwani wanashea baba mmoja.




 

“Jina langu kabisa naitwa Mohammed, baba yangu anaitwa Salum na babu yangu anaitwa Iddy halafu la ukoo unamaliza na lile la Nyange. Esma ni dada yangu upande wa Naseeb, kwa sababu Naseeb na Esma mama yao ni mmoja lakini mimi na Naseeb ni watoto wa baba mmoja. Kuna mambo ambayo watu wakubwa wameyaficha, hata kama nipo kwenye interview (mahojiano), mimi ni mtoto mdogo sipaswi kuyasema.



“Mwaka 1999, nikiwa Uwanja wa Kaunda pale Kariakoo nimekaa na wenzangu, akaja dogo mmoja pale anaitwa Evart, alikuwa amebeba mtoto akaniita akaniambia huyu ni ndugu yako, mtoto huyo alikuwa Naseeb, nilipomwangalia tu nikamwona kweli tunafanana, japo nilikuwa mkubwa lakini Diamond alinitangulia darasa.

 

“Nikaenda naye nyumbani, baba yangu (marehemu kwa sasa) alikuwa ameenda hospitali kumuona baba yetu mdogo ambaye alikuwa na tatizo la akili, baba alimpitia mama wakati ule Tandale, pamoja Diamond wakati wanakwenda kumuona mgonjwa.

 

“Walivyorudi wakaja mpaka Kariakoo wakanitambulisha huyu ni mdogo wako, nilifarijika sana na upendo ulikuwa mkubwa kuona tumepata ndugu yetu mwingine kwa maana sisi tupo watatu, mimi mkubwa, yupo Iddy na Asia wote ni baba mmoja na mama mmoja, alivyoongeza Diamond nilifurahi,” amesema Ricardo.



 

Baada ya kupigiwa simu, mama Diamond amefunguka haya: “Kama mnavyomwona Diamond na Ricardo Momo wanavyofanana, baba yao ni mmoja, anaitwa Salum Iddy na siyo Mzee Abdul. Diamond na Queen Darleen ni udugu kwa sababu ya baba mlezi.

 

“Mzee Abdul alikataa mimba ya Diamond tangu tumboni, akasema ‘hiyo mimba siyo yangu’, na yeye mwenyewe anajua na nilishamwambia. ‘Ungekubali mimba usingekosa mtoto’, hakutoa matunzo kuanzia nursery, primary mpaka sekondari. Mzee Abdul alinikuta na mimba ya Diamond ambayo nilitoka nayo kwa baba yake na Ricardo Momo, huo ndiyo ukweli na ndivyo ilivyo,” amesema Mama Dangote.