WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kufufua zao la mkonge nchini, hivyo amewataka Watanzania wachangamkie fursa hiyo  kwa kujenga viwanda vya kuchakata bidhaa mbalimbali zitokanazo na zao hilo kama sukari, dawa, vinywaji, mbolea na nyuzi.

Ametoa kauli hiyo jana (Alhamisi, Januari 21, 2021) wakati akizungumza na wananchi baada ya kukagua shamba la mkonge la Kigombe wilayani Muheza ambalo ni miongoni mwa mashamba ya mkonge yaliyo chini ya Kampuni ya Amboni Plantation Limited.

Waziri Mkuu amesema wakati umefika kwa Watanzania wanaoishi katika maeneo ambayo zao la mkonge linastawi wachangamkie fursa hiyo kwa sababu zao hilo linalimwa na watu wote na si kilimo cha matajiri peke yake.

Amesema awali watu waliaminishwa kwamba zao la mkonge ni zao linalolimwa na watu wenye uwezo mkubwa mkubwa kifedha na wengine walibaki kuwa vibarua jambo ambalo si kweli. “Wote tunaweza kulima mkonge na Serikali imejipanga kuhakikisha zao hili linalimwa na watu wote, amua sasa na utaona faida yake.”

“Mkonge ni utajiri, mkonge ni fedha ya uhakika na mkonge ni zao ambalo mzazi akiwekeza kwa ajili ya mtoto wake litamsaidia hapo baadaye hata kama yuko darasa la saba, mkonge atakaoupanda leo utamsomesha hadi chuo kikuu.”

Waziri Mkuu amesema kwamba mkulima wa kawaida anaweza kuanza kulima hata ekari moja, ambayo atapanda jumla ya miche 1,600 na baada ya miaka mitatu atavuna tani moja na nusu hadi mbili iwapo shamba litasimamiwa vizuri. Bei ya tani moja ya mkonge wa daraja la juu ni sh. milioni nne.

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka vijana kujikita katika kilimo hicho na pia waanzishe vitalu vya miche ya mkonge na kuiuza kwa wakulima kwa sababu mahitaji yameongezeka baada ya Serikali kufufua zao hilo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Amboni Plantation Limited, Casbert Nail amesema wameajiri watumishi 2,490 katika mashamba yao matatu, Mwera Estate (901), Sakura Estate (832) na Kigombe Estate (757).


 (mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU